Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amepongeza Mkoa wa Pwani kwa mafanikio makubwa katika sekta ya viwanda chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Mhe. Abubakar Kunenge.
Msigwa alitoa pongezi hizo leo wakati wa ziara yake katika eneo la Vigwaza, Wilaya ya Kibaha, ambapo alitembelea kongani ya viwanda ya Sino Tan kabla ya kufanya mkutano na waandishi wa habari wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam katika Bandari Kavu ya Kwala.
Ningependa kuwashukuru uongozi wa Mkoa wa Pwani chini ya Mhe. Abubakar Kunenge kwa juhudi kubwa katika kuhamasisha uwekezaji wa viwanda. Kama mnavyoona, ndugu waandishi wa habari, bidhaa kama majokofu, vilainishi, na maduveti yanazalishwa hapa,†alisema Msigwa.
Amebainisha kuwa Mkoa wa Pwani umepokea miradi 369 ya uwekezaji, ambapo asilimia 67 ni miradi ya viwanda, ikifikia idadi ya viwanda 247. Kiasi cha uwekezaji kilichowekezwa na sekta zote katika mkoa huo ni dola za Marekani bilioni 4.6, huku asilimia 61 ya mitaji hiyo, sawa na dola bilioni 2.8, ikitokana na sekta ya viwanda.
Kuhusu mradi wa kongani ya viwanda wenye ukubwa wa ekari 2,500, Msigwa alisema mradi huo una mtaji wa uwekezaji wa dola za Marekani milioni 327. Pindi utakapokamilika, kongani hiyo inatarajiwa kuwa na viwanda vikubwa na vya kati 200, pamoja na viwanda vidogo 300 vinavyohusika na usindikaji wa vyakula, utengenezaji wa vifaa vya ujenzi, viwanda vya dawa, usindikaji wa ngozi na nguo, pamoja na viwanda vya kemikali.
Alieleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa awamu tano, ambapo awamu ya kwanza imefikia asilimia 80. Kukamilika kwake kunatarajiwa kuleta ajira za moja kwa moja 100,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 500,000.
Hadi sasa, viwanda vitatu tayari vinafanya uzalishaji, vingine vitatu vipo katika hatua za mwisho za kufunga mitambo, huku viwanda vinne vikitarajiwa kuanza ufungaji wa mitambo kufikia Aprili 2025, aliongeza Msigwa.
Aidha, eneo hilo linatarajiwa kuzalisha bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 6 kwa mwaka na kuchangia mapato ya kodi na ushuru yanayokadiriwa kufikia shilingi trilioni 1.2 kila mwaka.
Kuhusu Bandari Kavu ya Kwala, Msigwa alifafanua kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kupunguza msongamano wa meli katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kurahisisha upakuaji na usafirishaji wa mizigo. Alisema bandari hiyo tayari imeanza kufanya kazi na mpaka sasa imepokea makontena 700.
Aliongeza kuwa mradi wa Bandari Kavu ya Kwala unatekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya shilingi bilioni 83.246.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji na uboreshaji wa miundombinu, ikiwemo bandari mbalimbali nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.