Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amehitimisha rasmi kambi ya matibabu ya macho iliyodumu kwa siku tatu, ikiwa na lengo la kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Mkuranga. Kambi hiyo ilitoa huduma za utoaji wa miwani, dawa za macho, ushauri wa kitaalamu, pamoja na upasuaji wa mtoto wa jicho.
Huduma hizo zilitolewa na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Bilal Muslim Mission of Tanzania kwa kushirikiana na Beta Charitable Trust (UK), Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo, na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Mhe. Abdallah Hamis Ulega. Kambi hiyo ilifanyika katika Shule ya Msingi Mkuranga na Shule ya Msingi Kizapala, ikiwafikia mamia ya wananchi wenye mahitaji ya huduma za macho.
Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo leo, Desemba 9, 2024, Mhe. Kunenge aliishukuru taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania kwa kutoa huduma bure kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani, hususan katika Wilaya za Bagamoyo na Mkuranga. Alitoa wito kwa taasisi hiyo kuendelea kushirikiana na serikali ili kufikisha huduma hizi muhimu katika wilaya nyingine za mkoa huo.
Aidha, Mhe. Kunenge alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira wezeshi yanayoruhusu taasisi binafsi kushirikiana na serikali katika kuboresha maisha ya wananchi. Pia alimpongeza Mhe. Abdallah Hamis Ulega kwa mchango wake katika kufanikisha kambi hiyo, huku akimshukuru Rais kwa kumteua Mhe. Ulega kuwa Waziri wa Ujenzi.
Kambi hii ni mfano wa mafanikio ya ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha huduma za msingi za afya zinawafikia wananchi wengi zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.