Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amesema maandalizi ya hafla ya uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala pamoja na miradi mingine mikubwa ya kimkakati yamekamilika, huku akitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo muhimu.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 30, 2025 katika eneo la tukio, Kunenge alisema uzinduzi huo utafanyika Julai 31, 2025, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza kuwa katika Kongani ya Viwanda ya Kwala eneo linalotajwa kuwa miongoni mwa maeneo makubwa ya viwanda Afrika Mashariki .
Ameeleza kuwa Rais Samia atazindua viwanda saba ambavyo tayari vimekamilika na kuanza uzalishaji, pamoja na kutembelea viwanda vitano vilivyopo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Aidha, Kunenge amesema kuwa safari rasmi ya treni ya mizigo kupitia reli ya kisasa ya SGR itazinduliwa katika Kituo Kikuu cha kuunganishia mabehewa (Marchalling Yard) na karakana maalum ya matengenezo ya treni hizo, zote zikiwa ndani ya eneo la Kwala.
Akizungumzia Bandari Kavu ya Kwala, Kunenge alisema mradi huo utaongeza ufanisi mkubwa katika shughuli za usafirishaji wa mizigo kwa kuhudumia wastani wa makasha 823 kwa siku, sawa na zaidi ya makasha 300,000 kwa mwaka. Hatua hii inatarajiwa kupunguza kwa zaidi ya asilimia 30 msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam.
Katika tukio hilo pia, Rais anatarajiwa kupokea mabehewa 160, ambapo mabehewa 100 ni mapya yaliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya reli ya MGR, mabehewa 20 yamefanyiwa ukarabati, na mabehewa mengine 40 yametolewa na Shirika la Chakula Duniani (WFP).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.