Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist W. Ndikilo ameunda kamati maalum ya kuchunguza tatizo la ongezeko la utoro kwa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari katika Mkoa wa Pwani.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa kilele cha maadhimisho ya juma la Elimu Mkoa wa Pwani lililofanyika Wilayani Mkuranga. Mhe. Ndikilo alisema kuwa amelazimika kuunda kamati hiyo baada ya tatizo la utoro kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuzidi kuongezeka kwa kasi kubwa hasa kuanzia mwaka uliopita.
Aidha alisema kuwa kamati hiyo ambayo imeanza kufanya kazi tarehe 09/05/2017 imepewa jukumu kubwa la kuchunguza kwa kina sababu zinazopelekea wanafunzi kutohudhuria shuleni wakati serikali imeondoa michango yote katika sekta ya Elimu pamoja na shughuli wanazofanya wanafunzi hao ili wasije wakawa wanakatishwa masomo na kwenda kujiunga na makundi ya uhalifu.
Pia amekemea tabia ya baadhi ya wazazi ambao wanakwamisha jitihada za Serikali kuinua kiwango cha Elimu na ufaulu kwa kuwashawishi watoto wao kuandika majibu ya uongo wakati wa darasa la saba ili wasifaulu. Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, katika kipindi cha miaka miwili zaidi ya wanafunzi elfu mbili ni watoro shuleni na wengine wamekatisha kabisa masomo.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Pwani Bi. Germana Mng’aho amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ya utoro wa rejareja kwa wanafunzi na Sekondari bado sekta ya Elimu katika Mkoa wa Pwani inakabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu pamoja na uhaba wa vyumba vya madarasa jambo ambalo linasababisha baadhi ya wanafunzi kusomea nje chini ya miti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.