Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga, amewaagiza Maafisa Elimu wa Mkoa wa Pwani kuratibu kwa ufanisi utaratibu wa upandaji miti katika shule zote za Mkoa huo. Amewataka kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapoanza shule anakuwa na mche wake wa mti, ili kuboresha mazingira na kudumisha upatikanaji wa lishe bora.
Mhe. Ndemanga aliyasema hayo leo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, katika maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti Kimkoa yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Chalinze Mzee, Halmashauri ya Chalinze. Katika maadhimisho hayo, alishiriki pia katika zoezi la upandaji wa miti 560.
Aidha, alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, Mkoa wa Pwani ulipanda miti 10,436,494 katika Halmashauri zote ikihusisha mashamba ya watu binafsi , vikundi na Taasisi mbalimbali za Kiserikali na zisizo za Kiserikali sawa na asilimia 77.3 na Katika msimu huu wa mwaka 2024/2025 jumla ya miche 10,517,135 imepandwa sawa na asilimia 77.9 ya lengo la miti milioni 13 na laki tano kwa mwaka.
“Hatuna sababu ya kushindwa kufikia asilimia 100. Tuhakikishe kila Halmashauri inapanda miti 1,500,000 ili kufikia lengo hilo,” alisema Mhe. Ndemanga.
Vilevile, alizitaka taasisi za Serikali na zisizo za Serikali kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika upandaji wa miti na kupata huduma za kitaalamu ili kuweka mikakati madhubuti ya utunzaji wa miti yote iliyopandwa.
Mhe. Ndemanga pia aliwataka wataalamu kutoka ngazi za Mkoa na Wilaya kushirikiana katika kutoa huduma za kitaalamu za kukabiliana na ugonjwa wa mchwa ambao umekuwa ukiathiri miti baada ya kupandwa.
Aliongeza kuwa kila shule inapaswa kuwa na kitalu cha bustani ya matunda kama njia ya kukabiliana na tatizo la lishe mashuleni. Aidha, alisisitiza kuwa kila taasisi iwe na vitalu vya miche ya miti.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji, Shangwe Twamala, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Machata, aliwataka wananchi kuendelea kudumisha utamaduni wa upandaji na utunzaji wa miti. Alipongeza pia ushiriki wa wanafunzi kwenye zoezi hilo, akisema watakuwa mabalozi wazuri wa utunzaji mazingira katika jamii zao.
Naye Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki, PCO Mathew Ntilicha, akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, alisema lengo kuu la upandaji miti ni kuhamasisha jamii kuhifadhi misitu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Alisema kuwa juhudi hizi zinaunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, ambaye pia ni Afisa Elimu Msingi, Bi. Miriam Kihiyo, aliwaagiza walimu wakuu wa shule kuhakikisha kila mwanafunzi anapanda na kutunza mti. Alisema Halmashauri hiyo ina zaidi ya wanafunzi 61,000, na akaomba TFS kuwasaidia dawa kwa ajili ya kuzuia athari za mchwa kwenye miti.
Afisa misutu kutoka Mkoa wa Pwani Piere Protas Ntiyamagwa akisoma risala kwa Mgeni rasmi alisema Vitendo vinavyofanywa na binadamu katika misitu mfano ukataji miti, fito na nguzo za ujenzi, uchomaji mkaa, uchimbaji mchanga, upasuaji mbao vimesababisha uoto wa asili (misitu) kupungua kwa kasi kubwa na Kutoa wito kushiriki katika zoezi la upandaji miti ili kukabiliana na madahara yatokanayo na changamoto hizo.
Aidha alisema shughuli za kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati mbadala zipewe kipaumbele katika kazi zetu za kila siku na kwenye mipango yetu ya maendeleo. Natoa rai kwa Serikali zote za Vijiji zinazouza maeneo wasiingilie maeneo yenye misitu hata kama hayajahifadhiwa kisheria.
Maadhimisho ya Siku ya Kupanda Miti hufanyika kila mwaka tarehe 21 Machi, na kwa mwaka 2025, yamebebwa na kaulimbiu: “Ongeza Thamani ya Mazao ya Misitu kwa Uendelevu wa Rasilimali za Misitu kwa Kizazi cha Sasa na Kijacho.”
ReplyReply allForward
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.