Madhara yaliyotokea kwa baadhi ya wakazi wanaoishi na kuendesha shughuli zao kando ya mto Rufiji yametokana na mto huo kujaa maji kufuatia mvua zilizonyesha hivi karibuni pamoja na maji yaliyotoka katika Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julias Nyerere.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alipokutana na kuzungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya suala hilo Machi 14, 2024.
Katika ufafanuzi wake, Kunenge amesema kutokana na mvua hizo bwawa hilo lilijaa maji na kufikia kina cha mita za ujazo 183.85 ambayo wataalamu walifikia maamuzi kuwa baadhi ya mageti yafunguliwe ili kuruhusu maji hayo kupungua ambayo kwa sasa yamefikia mita za ujazo 183.45.
Amesema kabla ya kufunguliwa mageti hayo, Serikali ilitoa taarifa kwa wananchi kwa kutumia njia mbalimbali za kimawasiliano ikiwemo kutangaza katika Redio ya Rufiji FM, nyumba za ibada na hata kupitia wenyeviti wa vjiji na vitongoji ili waweze kuchukua tahadhari dhidi ya madhara ambayo yangeweza kutokea na wengine walitii wakaondoka na hata kuokoa mazao yao.
"Baada ya mageti hayo kufunguliwa katika bwawa hilo, maji yamesambaa katika bonde la mto Rufiji na kuleta mafuriko ambayo yamesababisha kuwepo kwa athari kwa wananchi wanaofanya shughuli za kilimo pembezoni mwa mto huo," amesema.
Ameongeza kuwa "athari mojawapo iliyopatikana ni kuharibiwa kwa mazao baada ya kufunikwa na maji mengi, hata hivyo wengine walifanikiwa kuokoa mazao yao kwa kuwa waliwahi kuondoka mara baada ya kupewa taarifa juu ya kufunguliwa kwa maji hayo.
Kuhusu usalama wa wananchi katika eneo hilo, Kunenge amesema tayari vyombo vya uokoaji vimefanyakazi na sasa hali inaendelea vizuri na akasisiti kuwa tahadhari lazima ichukuliwe kwa kuwa mvua kubwa zinatarajiwa kuendelea kunyesha.
“Tunaendelea kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi kuwa waondoke katika maeneo hayo ili kuepusha vifo kwakuwa mvua nyingi zinatarajiwa kuendelea kunyesha hivyo kufanya mto Rufiji kuendelea kujaa maji,” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa amefafanua pia kuwa kamati ya maafa inaendelea kufanya tathmini katika maeneo yote ya Wilaya za Rufiji na Kibiti ili kuweza kujua athari iliyopatikana na kuitolea taarifa kwa wananchi.
Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julias Nyerere tayari limeanza kuzalisha megawati 235.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.