Mwenge wa Uhuru umekamilisha mbio zake katika Halmashauri ya Chalinze Aprili 10, 2025, ikiwa ni siku ya tisa tangu uzinduliwe katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani mnamo Aprili 2, 2025.
Katika mbio hizo, Mwenge wa Uhuru umepitia wilaya saba na halmashauri tisa, ukikagua na kuzindua jumla ya miradi 64 yenye thamani ya sh trilioni 1.028. Tarehe 11 Aprili, ambapo Mwenge huo utakabidhiwa Mkoani Morogoro.
Akiwa Halmashauri ya Chalinze Aprili 10, 2025, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, alikagua mradi wa machinjio ya kisasa ya Union Meat Abattoirs Ltd yaliyopo katika kijiji cha Kwazoka, Kata ya Vigwaza, mradi uliogharimu sh. bilioni 26.
Ussi aliwataka wafugaji kukimbilia fursa ya soko la ndani na nje kupitia machinjio hayo, akisema kuwa tofauti na miaka ya nyuma, sasa wafugaji wana uhakika wa soko kupitia uwekezaji unaofanywa ndani ya nchi.
“Haya yote ni matokeo ya jitihada pamoja na mapinduzi ya maendeleo yanayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na watendaji wa halmashauri, wilaya na wabunge,” alisema Ussi.
Aidha, alisifu uwekezaji mkubwa uliofanywa na Union Meat Group kwa kusogeza soko karibu na wafugaji wa ndani.
Mkurugenzi wa machinjio hayo, Mariam Mnghwani, alieleza kuwa yana uwezo wa kuchinja ng’ombe 300 kwa mstari mmoja kwa siku, pamoja na kondoo 3,000.
Pia, yana uwezo wa kuhifadhi hadi tani 150 kwa wakati mmoja na huzalisha tani tatu za nyama kwa siku, na bidhaa nyingine kama mifupa na ngozi zinazouzwa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Mnghwani, nyama inayozalishwa huuzwa ndani ya Tanzania na pia katika nchi za Qatar, Oman na Bahrain.
Katika siku hiyo hiyo, Ussi alizindua mradi wa maji katika vijiji vya Visezi (Chauru) na Pingo, unaotekelezwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), ambao unawanufaisha wakazi 2,822 kutoka kaya 565.
Mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na umetumia zaidi ya shilingi milioni 206.878, sawa na asilimia 68.78 ya bajeti, chini ya mkandarasi mzawa Sajo Civil Engineering & Building Construction Ltd.
Awali akipokea Mwenge huo kutoka Kibaha, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, alisema Mwenge wa Uhuru umetembelea miradi saba katika Halmashauri ya Chalinze yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 28.9.
Miradi mingine iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa vyumba 50 vya biashara katika kituo cha mabasi cha Chalinze, mradi unaotekelezwa na Halmashauri hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 216.5.
Vilevile, Mwenge umetembelea ujenzi wa shule ya Amali Msoga na mradi wa uwekaji wa taa 50 za barabarani katika kijiji cha Ruvu, Kata ya Vigwaza, uliogharimu sh.milioni 185.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.