Mwenge wa Uhuru umeendelea na mbio zake katika Mkoa wa Pwani, ikiwa ni siku ya sita tangu uzinduliwe rasmi na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango, tarehe 2 Aprili 2025.
Katika Wilaya ya Kibiti, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Joseph Kolombo, amesema Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukimbizwa umbali wa kilomita 119.8 huku ukitembelea, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye jumla ya miradi 13 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi milioni 610.1.
Akizungumza wakati wa mbio hizo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, amewapongeza wananchi kwa mwitikio mkubwa na jinsi wanavyojitokeza kuupokea Mwenge wa Uhuru katika maeneo yao.
Ussi pia ameeleza kufurahishwa na maendeleo yaliyofikiwa wilayani Kibiti, akisema yamekuwa yakitekelezwa kwa usimamizi mzuri wa Halmashauri pamoja na viongozi wa Wilaya. Ametoa wito kwa watendaji kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, uwazi na uwajibikaji.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zinaendelea kuhimiza ushiriki wa wananchi katika masuala ya maendeleo, pamoja na kutoa ujumbe wa kudumisha amani, umoja na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.