Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Simon Nickson, ameyahimiza mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanayofanya kazi mkoani Pwani kutoa elimu kwa jamii ili kuwajengea uwezo wa kutoa maoni na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa.
Hayo ameyasema Agosti 28,2024 wakati wa mkutano wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NacoNGO) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
“Tunawategemea sana katika kuhamasisha wananchi, kuongeza uelewa wao, na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kupiga kura. Aidha, tunategemea mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana nasi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii,” alisema Bw. Simon Nickson.
Aidha, aliipongeza NacoNGO kwa ushirikiano wake na serikali katika kutatua changamoto za wananchi, ikiwemo upatikanaji wa maji safi katika ngazi ya mkoa na kitaifa kwa ujumla.
Akiongea kwa niaba yay a katibu tawala Mkoa, Katibu tawala Msaidizi, Mhandisi. Felix Nlalio, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali na serikali, na pia kati ya mashirika yenyewe, ili kurahisisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Mhandisi Nlalio alieleza umuhimu wa mashirika hayo kutoa elimu kwa jamii na kuibua masuala mbalimbali yanayoweza kutoa dira ya maendeleo, huku akiwatahadharisha dhidi ya uchochezi na vurugu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NacoNGO), Jasper Makalla, alisisitiza umuhimu wa mashirika hayo kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kutoa ushirikiano katika kuwasilisha taarifa za kifedha ili kuwezesha mipango ya maendeleo.
Naye mjumbe wa Baraza hilo kutoka shirika la Mamas and Papas, ambaye pia ni Afisa Habari wa shirika hilo, Bw. Omary Kombe, alilishauri Baraza kuandaa kongamano la mkoa litakalowezesha mashirika kuonyesha shughuli mbalimbali wanazozifanya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.