Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta, leo amepokea ugeni kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya afya, Profesa Tumaini Nagu.
Ziara hiyo inalenga kufanya tathmini ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi, kukagua miundombinu ya afya, mifumo ya usimamizi, changamoto zinazowakabili watumishi wa sekta ya afya, pamoja na kupata mrejesho kutoka kwa wananchi kuhusu hali ya huduma zinazotolewa.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Prof. Nagu alisema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kuhakikisha kuwa huduma za afya zinatolewa kwa ubora unaostahili na kwa kufuata miongozo ya kisera ya Serikali.
Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, Prof. Nagu ametembelea Halmashauri ya Chalinze, ambako alikagua Kituo cha Afya cha Chalinze pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Chalinze iliyopo Msoga. Katika maeneo hayo, amekutana na watendaji wa sekta ya afya, watumishi wa vituo vya afya pamoja na wananchi waliokuwa wakipokea huduma, na kupata maoni yao kuhusu hali ya huduma.
Prof. Nagu anatarajiwa pia kutembelea halmashauri nyingine mbili za Mkoa wa Pwani ambazo ni Kisarawe na Rufiji, ambapo ataendelea na ukaguzi wa vituo vya afya na kuzungumza na wadau mbalimbali wa sekta ya afya.
Katibu Tawala wa Mkoa, Rashid Mchatta, amesema kuwa ugeni huo ni wa muhimu sana kwa Mkoa wa Pwani, kwani unatoa fursa ya kubaini maeneo yenye changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha huduma kwa wananchi.
“Tunaamini kuwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, tunaweza kuboresha zaidi huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, kwa wakati,” alisema Mchatta.
Ziara hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi kupitia uwekezaji katika miundombinu, rasilimali watu, na mifumo ya usimamizi wa sekta ya afya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.