Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mh. Mhandisi Evarist Ndikilo ametilia shaka ujenzi wa jengo la Mamlaka ya mapato Tanzania TRA Mkoa wa Pwani kwa kile alichoeleza kuwa muonekano wa jengo hilo hauendani na thamani iliyotajwa ambayo ni shilingi bilioni 2.6.
Pia ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Pwani kulifanyia uchunguzi suala hilo ili kuweza kubaini kama kuna ubadhilifu wowote uliofanyika wa fedha za Serikali.
Hayo yamebainika leo wakati wa Ziara yake ya ukaguzi wa majengo yaliyojengwa katika kitovu cha Halmashauri ya Mji Kibaha,ambapo alitembelea jengo la CRDB, Jengo la Uhamiaji Mkoa pamoja na Jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa haridhishwi na kasi ya ujenzi wa jengo la Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ambalo ilielezwa kuwa ujenzi wake ulianza mwaka 2015 ambapo hadi sasa bado halijakamilika huku tayari mkandarasi wa jengo hilo ameshalipwa asilimia 61 ya fedha za ujenzi wa jengo hilo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo kwa niaba ya Mkurugenzi , Meneja wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani bi Euvansia Lwiwa alisema Ujenzi wa Jengo hilo ulianza April 2015 na lilitakiwa kumalizika may 2016. Bi Euvansia alieleza kuwa ujenzi wa jengo hilo unatarajia kugharimu shilingi 2,693,402,120.60 pamoja na VAT ambapo mkandarasi wa jengo hilo Humphrey Construction ltd ameshalipwa takribani Shilingi 1,653,267,510.00 pamoja na VAT.
Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ni moja ya Tasisi ya Serikali ambayo ilipewa eneo la kujenga Ofisi katika eneo la kitovu cha mji cha Halmashauri ya Mji Kibaha ambapo mpaka sasa ujenzi wake haujakamilika.
Katika Hatua nyingine Mhandisi Ndikilo amezipongeza taasisi za Uhamiaji, Benki ya CRDB na NMB kwa kuweza kutekeleza Agizo la Waziri Mkuu kwa asilimia mia moja. Ikumbukwe kuwa Mhe.Waziri Mkuu alitoa agizo kwa taasisi zote zilizopewa viwanja katika kitovu cha Mji Kibaha kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.Mhe. Waziri Mkuu alitoa agizo hilo alipokuwa akifungua jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani Septemba, 2016.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.