Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka madiwani kuacha mara moja tabia ya kuingiza siasa kwenye shughuli za wataalamu katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa hospitali za Wilaya unaoendelea mkoani humo.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali unaoendelea katika halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Mhandisi Ndikilo amewataka baadhi ya wanasiasa na watendaji kutokukwamisha kwa namna yoyote miradi ya kitaifa na kimkoa kwa maslahi ya matumbo yao.
Mhandisi Ndikilo amezitaka halmashauri zinazotekeleza miradi ya ujenzi wa hospitali hizo ambazo ni Kibaha Mji, Kibiti na halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha kuwa wanakamilisha ujenzi huo ifikapo juni 25 mwaka huu na akasisitiza kuwa fedha zote zinazoelekezwa katika miradi hiyo muhimu zitumike kwa wakati na kwa matumizi lengwa bila kuziacha kubaki viporo.
"Uzoefu tulioupata juu ya kwanini tunachelewa chelewa sana ni kwa baadhi yetu kutaka fedha hizi, kuna watu wanajiwekea malengo ya kupata asilimia 10 kutoka kwenye hii hii bilioni 1.5, fundi wangu, mjomba wangu apate tenda ya ufundi, ndugu yangu alete matofali na kutusababishia kuchelewa malengo yetu"alifafanua mhandisi Ndikilo.
Nae mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama alieleza kuwa changamoto kubwa iliyosababisha kuchelewa kidogo kwa ujenzi ni hali ya mvua hivyo wanaomba kuongezwa muda japo siku 20 baada ya juni 25 mwaka huu.
Awali kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha Suzan Chaula alielezea kuwa wanajenga majengo saba ambapo ujenzi wa majengo yote umefikia asilimia 55.
katika kukabiliana na changamoto ya utoaji wa huduma ya afya kwa jamii serikali ya awamu ya tano inajenga hospitali za wilaya tatu za kisasa ,Mkoani hapa ambazo hadi kukamilika zitagharimu kiasi cha sh. bilioni 4.5.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.