Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo awataka waajiri na wafanyakazi kuheshimu sheria za utumishi wa umma kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi.
Mhe Ndikilo ameyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani yaliyoadhimishwa kimkoa katika halmashauri ya Mji wa Kibaha , katika viwanja vya shirika la Elimu Kibaha na kukemea tabia za baadhi ya waajiri wasiotaka kufuata sheria za utumishi kwa kunyanyasa wafanyakazi hatakuwa tayari kufanya kazi na watu wa aina hiyo katika Mkoa wa Pwani.
Akisoma Risala ya shirikisho la wafanyakazi(TUCTA )Mkoani Pwani Bwana Ramadhani Kinyagoli aliishukuru serikali kwa jitihada zake katika shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na serikali ya awamu ya tano kwa maslahi ya watanzania wakiwemo na wafanyakazi,hata hivyo hakusita kuwasilisha madai na changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi wa Mkoa wa Pwani ikiwa ni pamoja na wafanyakazi kutopandishwa vyeo kwa wakati,kodi kubwa ya mshahara,wastaafu kutolipwa mafao yao kwa wakati,waajiri kutoheshimu sheria za utumishi kwa kutowatendea haki watumishi kwa kuwapa maslahi yao kwa mujibu wa sheria,sekta binafsi kuwazuia watumishi kujiunga na vyama vya wafanyakazi na baadhi ya halmashauri kutoitisha vikao vya mabaraza ya wafanyakazi.
Kinyangoli aliendelea kufafanua kero zinazowasibu wafanyakazi katika Mkoa wa Pwani kwa kutoa shutuma kwa baadhi ya waajiri kutotimiza ahadi zao kwa wafanyakazi hodari wa mwaka jana kwa kutowapa zawadi zao hadi sasa na kuomba Uongozi wa mkoa ulifanyie kazi kwa waajiri hao kwani ahadi zisizotekelezeka kwa wakati huvunja moyo wa utendaji kazi kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na serikali.
Aidha Mhandisi Ndikilo aliwapongeza wafanyakazi hodari kwa mwaka 2018 kwa utendaji mzuri hata wakaweza kuteuliwa kuwa watumishi hodari kutoka katika taasisi zao .Aliendelea kulipongeza shirikisho la wafanyakazi mkoa wa Pwani kwa risala nzuri iliyosheheni mambo mazuri na yenye tija kwa mstakabari wa utumishi nchini na kusema hakika risala hii imejaa “Nondo za kutosha”Ndikilo alisema.
Pia aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazo wakabili wafanyakazi ambazo ziko ndani ya uwezo wake na kwa zile zilizo nje ya uwezo wake aliahidi kuziwasilisha kunakohusika kwa hatua zaidi. Aliwataka watumishi wa serikali na sekta binafsi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni katika utumishi sanjari na maadili ya kazi kwa mujibu wa taaluma walizonazo.Aliwataka wafanyakazi kujiepusha na matendo ya utovu wa nidhamu katika kazi.”Lazima tuwe na nidhamu ya kazi uvivu kazini ni sumu katika ajira”Ndikilo alisema.
Mhandisi Ndikilo alisikitishwa na kitendo cha waajiri wanaotoa ahadi hewa kwa watumishi hodari na kutowatunuku zawadi zao kwa wakati hili halikubaliki hata kidogo na kutoa onyo kwa waajiri wanaobagua wananchi katika ajira hususan watu wenye ulemavu na wanawake na alisisitiza sitakuwa tayari kufanya kazi na wawekezaji wa aina hii kwani wanafanya vitu vilivyo kinyume na katiba na sheria za nchi pia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.