Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Mhe.Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka wawekezaji wa viwanda kuhakikisha wanazingatia haki za wafanyakazi kwa kuwalipa maslahi yao kama inavyotakiwa bila la kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji na ubaguzi wowote kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zote za nchi kwa lengo la kutimiza azma ya serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda.
Kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi kwa ajili ya uwekaji wa mawe ya msingi katika kiwanda vitatu tofauti vya kuzalishia Nondo pamoja na mitungi ya Gesi vilivyopo Wilayani Kibaha,ambapo pia akusita kuwaasa watumishi na viongozi kuachana na vitendo vya urasimu kwa wawekezaji na badala yake watoe ushirikiano wa kutosha bila vikwazo vyovyote kwa lengo la kuleta chachu ya maendeleo kwa wananchi.
“Kwa sasa Mkoa wetu wa Pwani tunaendelea na kutekeleza agizo la Rais wetu Dk. John Pombe Maguli katika ujenzi wa viwanda mbali mbali, hivyo kitu kikubwa ninachowaomba wawekezaji wote wanaokuja kuhakikisha wanazingatia haki za wafanyakazi ili kuweza kutimiza malengo ambayo yamewekwa na serikali ya awamu ya tano ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,”alisema Mhandisi Ndikilo.
Aidha alibainisha kuwa wawekezaji ni chanchu kubwa ya kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi kutokana na wengine wao kuweza kupata fursa mbali mbali za ajira pindi viwanda vinapoanzishwa hivyo ni jukumu la watendaji na viongozi kuwa bega kwa bega na wadau wa maendeleo ili kuweza kuongeza zaidi ujenzi wa viwanda vingine.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa makampuni ya lake group Ally Awadhi lengo lao kubwa ni kumuunga mkono Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli katika ujenzi wa viwanda pamoja na kuwainua wananchi kiuchumi hasa ambao wanaoishi katika kaya ambazo ni masikini kuwapatia fursa za ajira.
Pia aliongeza kwamba kutokana na kuwepo kwa uwekezaji wa viwanda hivyo kutasaidia kuwainua wananchi wa Wilayani Kibaha pamoja na Mkoa wa Pwani kwa ujumla kutokana na kupata ajira ambazo zitasaidia kuwaongezea kipato sambamba na kuchangia katika ulipaji wa kodi amabazo zitafanya pato la Taifa kuongezeka.
Kukamilika kwa viwanda hivyo vitatu vya utengenezaji wa nondo,na chuma hususan cha kutengenezea mitungi ya gesi kutaweza kusaidia wananchi kwa kiasi kikubwa fursa za ajira pamoja na kupunguza changamoto ya ukataji wa miti ovyo kwa ajili ya kupata nishati ya mkaa ambayo imekuwa ni kero ya siku nyingi katika maeneo ya Mkoa wa Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.