Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa amesema, ataendelea kuwa mkali kwa mtumishi ambaye atakuwa mzembe katika suala la ukusanyaji na udhubiti wa mapato katika Halmashauri ya Chalinze.
Kawawa aliyasema hayo juzi wakati wa kikao Maalumu Cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kupokea taarifa ya hati ya ukaguzi wa hesabu za Halmashauri pamoja na Taarifa ya Utekelezaji wa Hoja za Ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Katika kikao hicho kilichofanyika Lugoba, Kawawa alisema mtumishi ambaye hawezi kusimamisha ipasavyo mapato ya Halmashauri ni vema akaomba kuhama.
"Nitaendelea kuwa mkali na mwiba kama kuna mtu anayefanya uzembe katika suala hili tusije tukalaumiana " alisema Kawawa.
Mkuu huyo wa Wilaya pia aliwataka watumishi wa Halmashauri hiyo kuacha kulindana kwa kuwaficha wanaosababisha ukusanyaji wa mapato kuyumba na pia kuepuka kuingia mikataba na mawakala wasio waaminifu.
Alisisitiza usimamimizi katika vyanzo vya mapato ili yasishuke, huku akitoa onyo kwa wakusanyaji kuzingatia taratibu na kupeleka fedha wanazokusanya benki badala ya kukaa nazo.
Akiwasilisha maagizo kutoka kwa mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ambaye alimwakilisha katika kikao hicho, Kawawa alisema Halmashauri hiyo imepongezwa kwa kupata hati safi kwa miaka minne mfululizo.
Alisema,Mhandisi Ndikilo pia ametoa agizo kwa Halmashauri hiyo kuepuka kuzalisha hoja kwa kuzingatia Sheria na kanuni, lakini pia ameelekeza kuimarisha kitengo Cha ukaguzi wa ndani ili kurahisisha kuibua hoja mapema na kuzifanyia kazi.
Akiongea katika kikao hicho, kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala alisema, kama kuna kesii za muda mrefu ambazo zinakuwa ngumu kuzitatua Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ishirikishwe.
Twamala alisema, Halmashauri hiyo inatakiwa kusimamia kikamilifu vikundi vilivyokopa virejeshe mikopo kwa wakati.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze Zainabu Makwinya alisema, kwa kipindi kinachoishia Juni 2019 mapendekezo ya hoja za Ukaguzi yaliyotolewa yalikuwa 44 , yaliyotekelezwa na hoja kufungwa ni 18 sawa na asilimia 41 na yanayoendelea kufanyiwa kazi kulingana na hoja ya mkaguzi ni 26 sawa na asilimia 59.
Zainabu ambaye ni Afisa Elimu msingi wa Halmashauri hiyo alisema kwa hesabu za mwaka 2018/2019 Halmashauri hiyo imepata hati ya ukaguzi inayoridhisha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.