Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda ameupongeza Mkoa wa Pwani kwa kuwa kinara katika ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.
Akifungua Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki mjini Morogoro, Mhe. Pinda ameeleza kuwa hakuna zao ambalo halikubali katika Kanda hiyo kwa kuwa Kanda hiyo ina hali ya hewa tofauti tofauti.
Ameeleza kuwa kauli mbiu ya Maonesho hayo isemayo "Vijana na Wanawake ni Msingi wa mifumo endelevu ya Chakula" inaakisi ukweli kuwa wanawake ni jicho muhimu katika Chakula ikiwemo lishe kwa watoto huku akifafanua kuwa kwa vijana ni lazima waanze jitihada leo ikiwemo kukabiliana na changamoto za kilimo na mfumo wake uwe wa mashamba makubwa na yenye tija na akabainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Kanda ya Mashariki ina vijana asilimia 36 ambayo iko juu ya asilimia ya Taifa ya asilimia 34, hivyo ni muhimu wakiandaliwa vyema kushiriki katika mifumo ya uzalishaji na kuliletea taifa maendeleo.
Mhe. Pinda ametoa rai kwa viongozi wa Mikoa ya Kanda ya Mashariki Kujipanga na programu ya Mradi wa "Build Better Tomorrow" Kwa kuainisha mashamba watakayopewa vijana pale ambapo watajitokeza kutaka kujiendeleza katika sekta hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge akitoa salaam za Mkoa na Kanda ya Mashariki ameeleza kuwa matarajio ya Mikoa hiyo ni kuhakikisha kuwa matarajio na matamanio ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yanafikiwa na akaongeza kuwa yeyote mwenye shaka na jitihada na kazi za Mhe Rais afike katika mikoa hiyo kujionea na kushuhudia hayo.
Akiuelezea Mkoa wa Pwani, Mhe. Kunenge amesema kuwa unaendelea kuhakisha vipaumbele vyake ni sahihi na vipaumbele hivyo ni Vipaumbele vya Mhe Rais.
Amesema juhudi za Mkoa wa Pwani ni kuanzisha mazao mapya ikiwemo Michikichi na Mpunga na kuwa mazao ya Ufuta na Korosho yameendelea kufanya vizuri katika Mkoa huo ikiwemo kiwango cha ubora wa daraja la kwanza kufikia asilimia 92 kwa msimu uliopita.
Ameeleza kuwa washiriki wa maonesho ya nane nane ya mwaka huu wa 2023 wameongezeka kutoka watu 477 hadi 589 ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 na kuwa dhamira ya Mikoa ya Kanda ya Mashariki ni kuchangia katika kulisha Tanzania na Dunia nzima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.