Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kilimo kupitia mpango wa kutengeneza kesho iliyobora yaani ‘BBT’ kwa vijana ili kuwa na idadi kubwa ya kundi hilo ambalo litasaidia upatikanaji wa uhakika wa chakula na kuongeza wigo wa kujiajiri.
Hayo yamesemwa a Agosti 27, 2023 na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akifunga mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania bara yaliyofanya kwenye ukumbi wa chuo hicho kilichopo Halmshauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani ambayo yamefanyika kwa siku sita kuanzia Agosti 22 hadi 27.
Amesema tayari serikali inatekeleza program mbalimbali za kilimo zinazowahusu vijana na kwamba muitikio ni mkubwa wa kujihusisha na kilimo ambacho amedai kinatoa fursa nyingi za vijana kujiajiri na kujipatia kipato.
Ameongeza kuwa katika kufanikisha hayo wakuu wa mikoa na makatibu tawala wamejengewa uwezo na kulisaidia kundi ili kuzitumia vyema fursa zinazopatikana katika maeneo yao kupitia kilimo.
“Kupitia program yetu ya Jenga kesho iliyobora yaani Building Better Tomorrow (BBT) ambayo inaratibiwa na Wizara ya Kilimo pamoja na ya Mifugo tumewajengea uwezo vijana wengi namna ya kulima kilimo chenye tija na ufugaji wa kisasa, tayari baadhi yao wamefuzu masomo na tayari wameanza kazi katika maeneo yao ni muhimu sasa wakuu wa mikoa muwasaidie amesema Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha amewataka wakuu wa mikoa na makatibu tawala kutatua kero zote za wananchi hususani suala migogoro ya ardhi ambalo limekuwa ni tatizo kubwa katika baadhi ya mikoa.
Awali Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema ili kufikia malengo ya Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi ni wakuu wa mikoa kusimamia kikamilifu miradi na ikamilike kwa wakati.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Godfrey Chongolo, akitoa salaam za Chama hicho wakati shughuli hiyo, amesema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuongeza morali ya utendaji kazi kwa viongozi hao, ili kuleta ufanisi na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Mhe. Rais, Chama Cha Mapinduzi ndiyo tuliopewa dhamana na wananchi mwaka 2020, kushika dola, kuunda Serikali na kusimamia na kuongoza nchi. Mafunzo haya ambayo yametolewa kwa Viongozi na watumishi wa Serikali yatawaweka kwenye utayari wa kutoa huduma bora na zenye ufanisi mkubwa.
“Tunakupongeza sana wewe kwa kutoa fursa ya mafunzo haya. Tunampongeza Waziri wa TAMISEMI na watendaji wote wa wizara kwa mafunzo haya. Tuliahidi kwa wananchi mwaka 2020 kuwa Serikali tutakayoiunda na kuisimamia itatoa huduma bora. Kundi hili ni kundi muhimu sana katika utekelezaji wa Ilani, maana ndilo linalopokea mafungu yote ya miradi na shughuli za maendeleo kwa ajili ya wananchi,” amesema Ndugu Chongolo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.