Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema mkoa wake utaendelea kusimamia maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha unaongeza mvuto kwa wawekezaji.
Hayo ameyazungumza Novemba 1,2024 wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika kiwanda cha Goodwill kilichopo Mkuranga, Kunenge alisema uwekezaji huo una faida kubwa kiuchumi na unaleta heshima kwa taifa, kwani bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na chapa ya “Made in Tanzania.”
Kunenge alieleza kuwa Mkoa wa Pwani una viwanda vingi vinavyochangia uchumi wa nchi, huku soko kuu la bidhaa hizo likiwa Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa wataendelea kulinda na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili bidhaa zinazozalishwa ziwe na mchango chanya kwa uchumi wa taifa na kuleta heshima kwa Tanzania kimataifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliahidi kuimarisha ushirikiano na Mkoa wa Pwani, si tu katika sekta ya viwanda, bali pia katika sekta nyingine muhimu kwa manufaa ya wananchi wa mikoa yote miwili. Chalamila alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, akitolea mfano wa kiwanda cha Goodwill kinachomilikiwa na mwekezaji kutoka China, kama alama ya juhudi kubwa za serikali kuvutia wawekezaji nchini.
Pia, Chalamila alikipongeza kiwanda cha Goodwill kwa kutoa ajira kwa wazawa na akasisitiza umuhimu wa kiwanda hicho kuendelea kuzalisha bidhaa bora na kurudisha sehemu ya faida kwa jamii kupitia uwajibikaji wa kijamii (CSR).
“Viwanda kama Goodwill ni muhimu kwa kuimarisha uchumi na kuongeza ajira. Tutahakikisha ushirikiano wetu na Mkoa wa Pwani unaendelea kuimarika kwa manufaa ya wote,” alisema Chalamila. Ushirikiano kati ya mikoa hiyo unalenga kuhakikisha viwanda na wawekezaji wanapata mazingira mazuri ya kufanyia biashara, hatua inayosaidia kukuza uchumi na ustawi wa jamii katika maeneo yote mawili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.