Serikali Mkoani Pwani imeweka mikakati kabambe ya kutenga maeneo kwa ajili ya kilimo cha kisasa na chenye tija ambacho kitajumuisha mazao ya kibiashara kwa lengo la kukuza uchumi.
Hayo yamebainishwa leo January 26, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge wakati wa halfa fupi ya kukabidhi matreka matatu kwa uongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Katika hafla hiyo, Kunenge amesema kwamba matreka hayo matatu ambayo wamepatiwa na Rais Dkt. Samia yatakuwa msaada mkubwa katika kuleta mapinduzi kwenye kilimo cha kisasa.
"Sisi kama Mkoa wa Pwani tumejipanga kuhakikisha kwamba tunajikita zaidi katika kuboresha sekta ya kilimo na kwa sasa tumepokea matreka haya kwa ajili ya halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, hivyo hatuna budi kumshukuru Rais wetu kwa hatua hii ya kutupatia matreka haya," amesema.
Amefafanua kwamba katika kumuunga mkono Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sasa wameanza kujikita katika kilimo cha mazao ya biashara yakiwemo mazao ya Pamba, ufuta, michikichi, korosho mihogo pamoja na mazao mengine ambayo yataweza kuleta mabadiliko katika kukuza uchumi.
Kunenge ameeleza kwamba Mkoa wa Pwani unataka kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo hivyo ana imani kubwa juu ya mabadiliko hayo katika halmashauri zote tisa zilizopo katika Mkoa wa Pwani.
Amewaomba viongozi wa halmashauri hiyo kuhakikisha kwamba wanayatunza vizuri matrekta hayo ili yaweze kudumu kwa kipindi kirefu ili kuweza kuwasaidia wakulima katika kilimo cha biashara.
Ameongeza kuwa katika kuendana na kasi ya mabadiliko Wilayani ya Rufiji, tayari kumeshafanyika uzinduzi wa zao la pamba na kwamba kutajengwa kiwanda kikubwa kwa ajili ya kuchakata zao hilo.
Sambamba na hayo, amempongeza kwa dhati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za hali na mali katika kukuza sekta ya kilimo na kuwezesha upatikanaji wa matreka hayo.
Pia amesema kuwa wapo katika mikakati ya kujenga skimu kubwa za umwagiliaji ambazo zitaweza kuwasaidia wakulima katika kuendesha shughuli zao za kilimo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon amesema kwamba wameshakubaliana kuwa matrekta hayo yanakabidhiwa katika halmashauri ya Wilaya ya kibaha ili kuboresha kilimo cha kisasa.
Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kwamba katika mpango wao wamekubaliana mambo matatu ikiwemo kuunganisha kilimo pamoja na viwanda, rasilimali watu pamoja na teknolojia lengo likiwa ni kuwasaidia wakulima kulima kilimo cha kisasa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Erasto Makala ameishukuru Serikali kwa kuweza kuwapatia matrekta hayo ambapo amesema kuwa lengo lao kubwa ni kutoka katika kilimo cha chakula na kujikita katika kile cha biashara.
Mkoa wa Pwani kwa sasa umejipanga kuunganisha kilimo pamoja na viwanda lengo ikiwa ni kutimiza azma ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hasssan kulisha dunia nzima kupitia sekta ya kilimo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.