Katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Mkoa wa Pwani umeanza rasmi kushirikiana na taasisi pamoja na wadau mbalimbali katika kutekeleza kampeni ya utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya malezi, makuzi na ulinzi wa mtoto.
Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa ambaye pia ni mratibu wa Dawati la Watoto, Bi. Roseline Kimaro, alisema kuwa elimu inayotolewa inahusu maeneo mbalimbali muhimu kama vile uwajibikaji wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha watoto wanapata malezi na makuzi bora. Pia, elimu hiyo inahusu haki za watoto, ukatili wa kijinsia na wa mitandaoni dhidi ya watoto, pamoja na athari za mila na desturi potofu zinazoweza kuathiri mwelekeo wa maisha ya mtoto.
Pia alitaja Maeneo mengine yanayogusiwa katika kampeni hiyo ni pamoja na ndoa na familia, ukiukwaji wa maadili katika jamii kama vile matumizi ya lugha zisizo na heshima.
Aidha, asilsema Maadhimisho yanalenga kuwaelimisha na kuwakumbusha wazazi au walezi na watoa huduma wote wajibu wao katika kutekeleza haki tano za msingi za mtoto ambazo ni haki ya kuishi kwa mtoto bila kukatisha uhai wake, haki ya kuendelezwa kielimu, kiutamaduni na vipaji vya mtoto, haki ya kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote, haki ya kushiriki kutoa maoni katika masuala yanayomuhusu mtoto kulingana na umri wake na haki ya kutobaguliwa kwa mtoto kutokana na hali yake.
Pia Bi. Kimaro alitoa wito kwa taasisi, mashirika na wadau wote wenye nia ya kutoa elimu hiyo muhimu kushirikiana na serikali ya mkoa ili kuhakikisha jamii inapata maarifa sahihi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto.
Kilele cha kampeni hii kinatarajiwa kufanyika tarehe 16 Juni 2025, katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, mkoani Pwani na Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2025 ni "Haki za Mtoto:Tulipotoka, Tulipo na Tuendako”. Kaulimbiu hii inaitaka jamii kutafakari upatikanaji wa haki za watoto tangu zilipoainishwa na Sera ya Maendeleo ya Mtoto mwaka 2008.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.