Maambukizi ya virusi vya UKIMWI mkoani Pwani yamepungua kutoka asilimia 5.9 na kufikia asilimia 5.5 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Katika hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo iliyowasilishwa na Katibu tawala Mkoa bi Theresia Mmbando inasema kuwa takwimu za utafiti wa viashiria vya virusi vya UKIMWI na UKIMWI nchini kwa mwaka 2016-2017 zinaonesha kupungua kwa kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 7 mwaka 2003 mpaka kufikia asilimia 4.7 mwaka 2017.
“Kiwango cha maambukizi na vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua katika Mkoa wa Pwani lakini Halmashauri ya Kibaha Mji, mkuranga na chalinze zinaonekana kuwa na maambukizi makubwa” alieleza Mhandisi Ndikilo.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa watu wanaoishi na Virusi vya ukimwi Mjini Kibaha Antonia Mango alisema kuwa zipo sababu zinazofanya maambukizi kuwa juu na akazitaja baadhi kuwa ni kuwepo mwingiliano na watu kutoka nje ya Mji huo, madereva wa magari makubwa kuwa na nyumba ndogo katika baadhi ya vituo, ngoma za usiku kama vile za vigodoro, mikesha ya usiku nyakati za sikukuu, ngono zembe na ulevi uliopindukia.
Mango aliongeza kuwa sababu zingine ni pamoja na maonesho ya picha za ngono kwenye vibanda vya makuti katika mitaa, kwenye mitandao na cd, ubakaji na ulawiti pia baadhi ya wazazi wanaozaa watoto wenye VVU kutowaambia hali za kiafya watoto wao.
Maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani kimkoa yalifanyika katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha nakauli mbiu ambayo ni “Jamii ni Chachu ya Mabadiliko , Tuungane kupunguza maambukizi mapya ya VVU.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.