Mkoa wa Pwani umelazimika kubadili baadhi ya miradi itakayopitiwa na kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru kutokana na changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko kwenye baadhi ya maeneo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameyasema hayo leo April 25, 2024 ofisini kwake wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya maandalizi ya mapokezi ya Mbio za Mwenge wa huru Mkoani humo.
Amesema kuwa licha ya changamoto ya mafuriko katika baadhi ya maeneo, mkoa huo umekamilisha maandalizi kulingana na vigezo vilivyobainishwa ambapo Mwenge huo utapokewa April 29, 2024 kwenye viwanja vya Bwawani ukitokea mkoani Morogoro na kuwa wapo vizuri kuhakikisha Mwenge unakimbizwa maeneo yote yaliyopangwa kupitiwa.
"Mwaka jana mkoa wetu ulikuwa wa 12 Kitaifa, miradi ilikuwa 99 yenye thamani ya zaidi ya sh. trilioni 4.4, kwa mwaka huu tumejizatiti kufanya vizuri zaidi," amefafanua Kunenge na akawahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha mapokezi na mbio za Mwenge katika mkoa huo.
Ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru bado upo Mkoani Morogoro na unatarajiwa kupokewa mkoani Pwani april 29, 2024 ambapo utakimbizwa katika Halmashauri tisa hadi Mei 8 watakapokabidhi kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Kauli Mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2024, ni "Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu" ukiwa pia na jumbe zingine ambazo ni "Kuzuia Rushwa ni jukumu Lako na Langu; Tutimize wajibu wetu," "Jamii iongeze kutokomeza Ukimwi," "Ziro Malaria inaanza na Mimi - nachukua hatua kuitokomeza" na “Lishe sio kujaza Tumbo; Zingatia unachokula."
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.