Kiwango Cha ufaulu kwa mwaka 2022 kimeshuka Mkoani Pwan, kwa asilimia 1.174 ukilinganisha na matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2021.
Akizungumzia taarifa ya tathmini ya matokeo hayo, katika kikao kazi Cha kuboresha elimu ,Ofisa elimu Mkoani Pwani Sara Mlaki alieleza ,hali ya ufaulu katika mkoa kwa mwaka 2022 ni asilimia 83.162 ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2021 ambao ulikuwa ni asilimia 84.91 .
Ameeleza kuwa kushuka kwa matokeo hayo imetokana na changamoto ya baadhi ya wazazi kushawishi wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani Yao ya kumaliza elimu ya msingi 2022.
Aidha Sara , alieleza wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 47,906 wakiwemo wasichana 24,292 na wavulana 23,614, ambapo wanafunzi 47,453 wavulana 23,333 na wasichana 24,120 sawa na asilimia 99.05 walifanya mtihani.
"Wanafunzi 453 kati ya hao wavulana 281 na wasichana 172 sawa na asilimia 0.94 hawakufanya mtihani kwasababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro ,vifo na ugonjwa" .
"Jumla ya wanafunzi 39,463 wakiwemo wavulana 19,159 na wasichana 20,304 sawa na asilimia 83.162 walifaulu mtihani huo huku watahiniwa 7,990 wavulana 4,174 wasichana 3,816 ambao ni sawa na asilimia 16.838 hawakufaulu"
Ameeleza , mkoa unaangaliwa kwa Mazingira mazuri na bora Lakini inashangaza kwanini mkoa unashuka kiufaulu.
Sara alitaja sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu ni baadhi ya wanafunzi kuhamia shule za mkoa huo wakiwa hawajui kusoma ,kuandika na kuhesabu,uhaba wa walimu ,ukizingatia ongezeko la wanafunzi kufuatia Serikali kutoa elimu bila malipo.
Ametaja sababu nyingine kuwa ni baadhi ya walimu kutotimiza majukumu yao katika ufundishaji Kama vile kutokuwa na maazimio ya kazi,maandalio ya somo,nukuu za somo,zana za kufundishia na utoro kazini na udhaifu wa usimamizi na ufuatiliaji kwa baadhi ya maafisa elimu kata hali inayochangia ufundishaji na ujifunzaji kuwa wa kiwango cha chini.
Akifunga kikao hicho Katibu Tawala mkoani Pwani Zuwena Omari alielekeza ,wazazi wapewe elimu kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wao na walimu wasichoke kuongea na watoto kuhusu athari ya kufeli .
"Tuendelee kutoa elimu ya malezi kwa watoto na wazazi waendelee kupewa elimu ya kuthamini elimu kwa watoto wao bila kuchoka" mkoa huu una tamaduni zake ,kutokana na hilo tuongee na wazazi bila kuchoka hadi watakapobadilika "
Zuwena ameeleza, Serikali umejidhatiti kutatua changamoto na kuboresha masuala ya elimu kwa Raslimali watu ,fedha na miundombinu .
"Mkoa tumepata madarasa mengine 341 bado maeneo machache ambayo bado hawajamaliza ujenzi wapo kwenye hatua za umaliziaji ,tumeshuhudia mh.Rais dkt Samia Suluhu akijidhatiti kuondoa changamoto hizi za elimu ,wote tumeshuhudia akijenga madarasa mengi na Yale yaliyojengwa kupitia fedha za Uviko ambayo yalisaidia kupunguza msongamano madarasa"alisema Zuwena.
Kuhusu lishe Zuwena alisema kuna tatizo la lishe ,suala hilo lihimizwe na elimu itolewe kuhusu lishe kwa manufaa ya watoto na vizazi vijavyo.
Kuhamasisha jamii kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunzi ili kupambana na changamoto ya mahudhurio ya wanafunzi shuleni, kuboresha Mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa Halmashauri kuweka kwenye bajeti fedha za ujenzi wa miundombinu.
Zuwena ameeleza mkoa utasimamia utekelezaji wa mikakati iliyopangwa ili kuinua kiwango Cha ufaulu na kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.