Kikaocha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Pwani kiimepitisha mapendekezo ya Mpango na bajeti Shilingi Biln 298.5 ya mwaka 2021/2022 ambayo ni ongezeko la asilimia 9.38 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2020/2021.
Aliwasilisha rasimu ya mapendekezo ya bajeti katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Machi 15, mjini Kibaha, Mchumi katika ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Pwani Gerald Mbosori alisema utekelezaji wa Mpango na bajeti utaongozwa na dira ya Taifa ya Maendeleo ya miaka mitano.
Mbosori alisema vipaumbele vya Mkoa huo kwa mwaka 2021/2022 ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya Sekta ya Elimu na afya, kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani na uandaaji wa Mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji na ujenzi wa Viwanda.
Mchumi huyo alisema kwa mwaka 2020/2021 Mkoa huo uliidhinishiwa matumizi ya Shilingi Bilion 272.9 ambapo hadi kufikia Mwezi Desemba sekretarieti ya Mkoa huo imekusanya maduhuli ya Shilingi Bilion 3.7 sawa na asilimia 6.12 huku Halmashauri zikikusanya Shilingi Bilion 16.6 sawa na asilimia 43.04.
Pia aliongezea kuwa vipo vikwazo vinavyosababisha baadhi ya Halmashauri kutofikia malengo kuwa ni pamoja na wigo mdogo wa vyanzo vya mapato, usimamizi usioridhisha kwa baadhi ya vyanzo kama leseni za biashara, vileo na ushuru wa nyumba za kulala na upungufu wa vitendea kazi magari na pikipiki kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji.
Akifunga kikao hicho ambacho kilipitisha mapendekezo hayo ya bajeti Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alitoa wito kwa Halmashauri zote za Mkoani hapa kuhakikisha wanasimamia na kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani.
Ndikilo alisema uwepo wa vyanzo vya mapato vya ndani inasaidia kufanya miradi ya maendeleo kwa wakati bila kusubiri fedha kutokana Serikali kuu, huku akisisitiza wataalamu kuwa makini na kujenga uaminifu katika ukusanyaji wa mapato.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.