Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid MChatta, amepokea Kikombe cha Ushindi baada ya timu ya Mkoa wa Pwani kuibuka mabingwa wa jumla katika Mashindano ya Riadha ya Wanawake Ladies First, msimu wa sita. Mashindano hayo yalihitimishwa Novemba 24, 2024, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Wanariadha wa kike kutoka Filbert Bayi Sports Academy waliliwakilisha vyema Mkoa wa Pwani, wakitwaa ushindi wa kwanza miongoni mwa mikoa 31 ya Tanzania Bara na Visiwani. Nafasi ya pili ilinyakuliwa na Arusha, huku Kilimanjaro ikimaliza katika nafasi ya tatu.
Akizungumza baada ya kupokea kikombe, Bwana Rashid MChatta aliwapongeza wanariadha, walimu wao, na uongozi wa Filbert Bayi Sports Academy kwa juhudi zao za kukuza vipaji vya michezo mkoani hapa, hatua inayosaidia kuku kwa maendeleo ya sekta hiyo nchini.
Katika matokeo ya mchezaji mmoja mmoja mita 100 Siwema Matogoro (Pwani) amefanikiwa kukimbia 12:02, Bertha Evarest (Kilimanjaro) akikimbia kwa 12:21 na Elizabeth Victor (Arusha) ametumia 12:34.
Mita 200 Bertha Evarist (Kilimanjaro) amekimbia 25:39, huku Siwema Julius wa Pwani akikimbia kwa 25:41 na Aisha Thani wa mjini Magharibi akishika nafasi ya tatu kwa kutumia 26:52.
Matokeo mengine ni mita 400 Sharifa Mawazo wa Pwani amekimbia 58:53, huku Lucia Pius wa Pwani akishika nafasi ya pili kwa kutumia 58:71 na Magreth Fikiri wa Kilimanjaro kwa 59:07.
Pia katika mbio za mita 800 Sara Masalu wa Morogoro amekimbia 2:20:56, huku Salma Charles wa Pwani akikimbia 2:20:86 na Zahara Ramadhan wa Singida akitumia 2:21:53.
Kwa upande wa mita 1500 Neema Nyaisawa wa kilimanjaro amekimbia 4:40:07, huku Sara Masalu wa Morogoro akikimbia 4:44:36 na Zainab Issa wa Pwani akimaliza kwa 4:44:55.
Mashindano ya "LADIES FIRST" yalidhaminiwa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Japan (JICA) na kuratibiwa na Baraza la Michezo la Taifa kwa kushirikiana na Shirikisho la Riadha Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.