Mkoa wa Pwani umetekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kusafisha Bonde la Mto Ruvu ili kuwezesha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu.
Hayo yameelezwa leo Novemba 9, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge wakati akitoa taarifa kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdory Mpango juu ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Mkoa huo zikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayolenga kuondoa changamoto ya upungufu wa maji kwenye bonde hilo unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.
Mhe. Kunenge alisema kuwa ukaguzi wa Bonde hilo ulifanyika Novemba 2 na 3, 2022 kwa kutumia "Helkopter" na kubaini uwepo wa mifugo mingi huku kukiwa na uchepushaji Maji kwenye baadhi ya maeneo na kuwa tayari hatua zimechukuliwa kudhibiti hali hiyo.
"Baada ya kubaini hayo, tuliamua kuwaelekeza wale wote wanaotumia maji kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa njia halali (wenye vibali) wasitishe kwa muda, wasio na vibali pamoja na wenye mifugo kuacha mara moja na wameacha, lakini Operesheni zinaendelea, na kukamata watumiaji wasio na vibali na watakaokaidi maagizo na maelekezo haya," alifafanua Kunenge.
Akielezea taratibu walizotumia kufanikisha zoezi hilo, Mhe. Kunenge alibainisha kuwa ofisi yake ilitumia utaratibu mzuri wa kufanya mikutano na wadau mbalimbali iliyosaidia kubaini na kuthibiti uchepushaji wa Maji na kuzuia Ukataji Miti ili kutunza vyanzo vya maji.
"Katika kutekeleza Maagizo ya Mhe. Rais, niliitisha Mkutano wa Viongozi wa Mkoa ulioshirikisha Chama cha Wafugaji, Chama cha Wavunaji Mkaa, Viongozi wa Bonde la Wami RUVU na Wakala wa Huduma za Misitu na nnashukuru Waziri wa Maji alihudhuria na kikao hicho kikaweka mikakati ya kuhifadhi mazingira kwa kutoharibu vyanzo vya maji na kuzuia ukataji haramu miti."
Kuhusu udhibiti ukataji miti na kuchoma mkaa ovyo, Mhe. Kunenge alieleza kuwa mkoa wa Pwani umeazimia kudhibiti vyombo vya usafiri (pikipiki) vinavyobeba Mkaa kwa kuvisajili na kuvifuatilia kujua wanakotoa huo mkaa na kuwa wanapanga kuja na mpango wa kudhibiti uvunaji wa Mkaa kwa kupunguza utoaji vibali vya mkaa na hili litahamasisha matumizi ya nishati Safi ya gesi.
Kwa upande wa Ufugaji, alieleza kuwa kuna changamoto kubwa ya Mifugo vamizi na hasa katika kipindi hiki cha Ukame ambacho hata Mifugo iliyopo kwenye maeneo hayo wanatafuta maji.
"Katika hili, viongozi kutoka kwenye Mikoa yenye mifugo mingi tumekubaliana kuwa wafugaji wabakize mifugo yao kwenye maeneo yao na itambuliwe ili kuweka mikakati ya upatikanaji Malisho na Maji huku mikakati ya kuhuwisha matumizi bora ya ardhi, kuanzisha na kutumia Ranchi ndogo ndogo ikiendelea.
Makamu wa Rais alitembelea chanzo na mitambo ya maji ya Ruvu chini iliyopo katika Kijiji cha Kongo Kata ya Yombo Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani kujionea hali ya upatikanaji wa maji ulivyo kwenye Bonde la Mto Ruvu unaotegemewa na Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.