Kisarawe, Pwani – Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kutoa fedha za kutosha kuboresha sekta ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza Aprili 3 wakati wa ukaguzi na uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa maji wa Msanga, unaohudumia vijiji vya Bembeza na Chale, Kisarawe, Ussi alisema mradi huo wenye thamani ya Shilingi milioni 416 umekamilika kwa asilimia 70 na utanufaisha wakazi 2,449.
“Mradi huu ni mzuri, kazi zilizobaki zikamilishwe haraka ili wananchi wapate huduma ya maji safi, salama na yenye uhakika,” alisema Ussi.
Aliongeza kuwa maji ni hitaji la kila siku, hivyo Rais Samia ameendelea kushusha fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji ili kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi.
Aidha, Ussi aliwataka watendaji wa serikali kuendelea kumuunga mkono Rais katika juhudi zake za maendeleo na kuinua uchumi wa wananchi. Pia alipongeza usimamizi wa mradi huo kwa kutumia mfumo wa kidijitali wa manunuzi ya umma (NEST), unaosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA).
Katika hotuba yake kupitia Mwenge wa Uhuru, Ussi aliwahimiza wananchi kushiriki kwa utulivu na amani katika uchaguzi mkuu ujao na kuepuka vitendo vya rushwa ili kuhakikisha viongozi bora wanachaguliwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.