Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amebatilisha na kutengua umiliki wa shamba namba 934 lililokuwa mali ya AZANIA Investment Ltd, kitongoji cha Kiembeni Kata ya Mapinga, Bagamoyo Mkoani Pwani lenye ukubwa wa hekari 374 na kuamua kulirejesha Serikalini.
Eneo hilo liliingia katika mgogoro mkubwa na wananchi wavamizi ambapo awali AZANIA alitambulika ni mmiliki halali lakini mwishoni mwa wiki Rais Samia ilimpendeza kubatilisha eneo hilo.
Akiwa katika muendelezo wa ziara yake Kata ya Mapinga kutatua migogoro iliyokithiri, Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge alieleza kuwa kutokana na kutenguliwa kwa umiliki wa AZANIA kitongoji cha Kiembeni, inatafsiriwa wananchi bado ni wavamizi.
Kunenge alieleza kuwa kwa sasa hatua inayosubiriwa ni muongozo wa Rais na kuwa endapo itampendeza liwe eneo la makazi litákuwa chini ya Halmashauri ili eneo lipangwe.
Mkuu huyo wa mkoa alifafanua hakuna aliye juu ya sheria, kwa wale wote waliohusika na uuzaji holela na utapeli wa viwanja Mapinga wachukuliwe hatua za kisheria.
Nae mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Muharami Mkenge alieleza tangu mwaka 2021 alianza kusimamia kero hizo na sasa kata ya Makurunge matokeo yameanza kuonekana.
Awali mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash alitoa rai kwa wananchi kuacha kuuza ardhi kiholela na yeyote aliyeuziwa ardhi apate hati ya halali ili kujiepusha na migogoro.
Kwa upande wa wananchi mzee Bole Shindika amesema msimamo wa Serikali lazima uheshimiwe, wanashukuru Rais kwa hatua ya kwanza aliyoichukua na wanasubiri muongozo wake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.