Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia na kutoa eneo la ekari 5520 sawa na hekta 2208 za Ranchi ya Ruvu iliyopo mkoani Pwani ili itumike na wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kilimo, ufugaji na makazi.
Rais Dkt. Samia amefikia Uamuzi wa kutoa na kugawa eneo hilo ambalo ni sawa na hekta 2208 baada ya Tume iliyoundwa na Serikali kushughulikia migogoro ya ardhi nchini mwaka 2019/ 2020 kuleta mapendekezo ya namna ya kukabiliana na migogoro nchini.
Akikabidhi eneo hilo kwa viongozi wa maeneo hayo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde alitoa kauli hiyo kwa niaba ya Waziri wa Mifugo, Abdallah Ulega alipozungumza na wananchi waliofika kwenye hafla ya utiaji saini hati za makabidhiano kati ya Wizara yake na halmashauri za Chalinze, Bagamoyo na Kibaha iliyofanyika Mei 27, 2023 kwenye ukumbi wa (shamba la mifugo NARCO) Ranchi ya Ruvu.
Alisema kuanzia sasa ekari 5520 zitakuwa mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Chalinze na Kibaha ambapo viongozi watayagawa maeneo hayo kulingana na mahitaji ya wananchi.
Aliyataja maeneo yaliyotolewa na serikali kuwa ni Ruvu- Darajani hadi Bagamoyo ekari 500, Kidogozero ekari 500, Milo ekari 1000, Kitonga 1200, Kidomole ekari 100, Fukayosi ekari 100, Mkenge ekari 100, Magurumali ekari 500, Mperamubi au waya ekari 1500 na vigwaza ekari 20.
“Kutokana na uvamizi mkubwa uliofanywa na wananchi wanaozunguka ranchi hii, mwaka 2019/2020 serikali iliunda tume shirikishi ya kitaifa ya kushughulika na migogoro ya ardhi kuzunguka vijiji 16 vinavyopakana na ranchi ya Ruvu kwa ajili ya kufanya uhakiki na kurudisha mipaka halisi ambayo ilipimwa awali, pia ilifanya tathmini ya mahitaji ya ardhi, uvamizi na kushauri namna bora ya kushughulikia maombi ya wananchi juu ya kumiliki ardhi ili kumaliza migogoro.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya majukumu ya wizara katika kudhibiti uingiaji holela wa mifugo kutoka maeneo mbalimbali, kutatua migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, kusambaza teknolojia sahihi za ufugaji bora ili kuongeza uzalishaji wenye tija na kuchochea uwekezaji katika sekta ya mifugo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali wananchi wa Pwani na kwamba licha ya kuwa walivamia eneo la ranchi lakini Rais Dkt. Samia ameridhia kugawa sehemu ili iendelee kutumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
“Wananchi waliingia eneo ambalo linamilikiwa na serikali na kufanya shughuli za kibinadamu, tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan bila kujali ni kosa kisheria kuvamia eneo la ranchi lakini ameamua kuwamegea ili muendelee na shughuli zenu kwa nia ya kuhakikisha mnakuwa na hali bora kuendesha maisha yenu,” alisema Kunenga.
Hata hivyo Kunenge alionya kuwa baada ya kumega eneo la ranchi sasa ni marafuku kwa mwananchi yeyote kuvamia eneo lingine na kwamba atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo kwa kuruhusu sehemu ya ranchi ya Ruvu kupewa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo kilimo na ufugaji.
Alisema watahakikisha maeneo hayo yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa kama vile kilimo ambacho kitakuwa cha kisasa pamoja na ufugaji wa kibiashara ili kuwanufaisha wananchi wa maeneo hayo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Pwani, Ngobere Msamau alisema kuwa kwa niaba ya wafugaji amepokea kwa furaha kubwa na katika kuthamini walichokipokea watakwenda kuisimamia na kuitunza ranchi hiyo ya Ruvu ili waendelee kunufaika na fursa mbalimbali zinazoendelea kutolewa na serikali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Milo, John Simba alisema eneo lake lilikuwa na tatizo kubwa la migogoro ya ardhi hivyo ugawaji wa ardhi yenye ukubwa wa ekari 1000 itasaidia kukabiliana na adha hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.