Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge, amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa mfano bora wa kuigwa katika utendaji kazi, na hivyo kuwataka wafanyakazi wote nchini kuiga mfano huo.
Kunenge aliyasema hayo leo katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika katika uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani.
Alisema kuwa Rais Samia amekuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto za wananchi, jambo linalopaswa kuwa dira kwa wafanyakazi wote.
“Niwaambie, Mheshimiwa Rais ni mfanyakazi namba moja. Tunamwona anafanya kazi bila kupumzika, ametuwekea sera nzuri ambazo tunaona matokeo yake katika huduma bora za afya, elimu, uwekezaji, kilimo, mifugo, maji na miundombinu mingine. Hivyo basi, tusimuangushe,” alisema Kunenge.
Aidha, aliwataka watumishi wa sekta ya umma na binafsi kutokuwa na moyo wa kushindwa, akisisitiza kuwa hata Rais haamini katika kushindwa.
“Mhe. Rais haamini katika kushindwa, mimi pia siamini katika kushindwa, na Mkoa wangu hauamini katika kushindwa,” aliongeza.
Kuhusu maendeleo ya Mkoa, Kunenge alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano, mkoa wa Pwani umepokea shilingi trilioni 1.53 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Alisema fedha hizo zimetumika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na miundombinu.
Akizungumzia sekta ya viwanda, Kunenge alieleza kuwa mkoa huo una zaidi ya viwanda 1,500, ikiwa ni pamoja na viwanda vikubwa 78 ambavyo vimechangia kuongeza ajira kwa wananchi.
Aidha, alieleza kuwa mkoa umeanza mazungumzo na wawekezaji kuhusu utoaji wa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi pamoja na kuwahimiza wachangie kwenye mifuko ya jamii.
Akijibu risala ya wafanyakazi, Kunenge alitoa wiki moja kwa kila taasisi iliyotajwa kwenye risala hiyo kuwasilisha majibu ya changamoto zilizowasilishwa, hasa kuhusu mikataba ya ajira.
“Kama mikataba haipo, tujue ni nani anayesimamia. Ninachotaka kuona ni mikataba kuwepo na kila kero iliyotajwa hapa kuwa na majibu,” alisema Kunenge.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Pwani, Ramadhani Kinyogori, alishukuru Rais kwa kuendelea kutatua changamoto za wafanyakazi nchini.
Awali, akisoma risala ya wafanyakazi, Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Pwani, Bi. Susan Shesha, aliipongeza Serikali kwa kusikiliza na kutekeleza uanzishaji wa mabaraza ya wafanyakazi katika wilaya zote za mkoa huo, na pia kutoa huduma bora kwa watumishi mahala pa kazi.
Hata hivyo, Shesha alitaja changamoto zinazowakabili wafanyakazi kuwa ni pamoja na mishahara isiyoendana na hali halisi ya maisha, baadhi ya waajiri kukiuka mikataba ya ajira, kuwazuia wafanyakazi kushiriki sherehe za Mei Mosi, na kutotoa michango katika mifuko ya jamii.
Alisisitiza kuwa vyama vya wafanyakazi vinawaomba waajiri kutimiza wajibu wao na kuongeza kasi ya kulipa madeni ili kuepusha migogoro kazini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.