Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala, Mkoani Pwani, Julai 31, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 22, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Abubakar Kunenge, amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo kubwa la kihistoria.
Katika ziara hiyo, Mhe. Rais Samia atazindua rasmi safari za Treni ya Mizigo kwa njia ya Reli ya Kisasa (SGR), kupokea mabehewa ya mizigo kwa njia ya Reli ya Zamani (MGR), pamoja na kuzindua Kongani ya Viwanda ya Kwala (Kwala Industrial Park), moja ya maeneo ya viwanda makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Mhe. Rais atafanya uzinduzi rasmi wa safari za treni ya mizigo ya mwendo kasi kupitia Kituo Kikuu cha Kuunganishia Mabehewa ya Mizigo na Karakana ya Treni za Mizigo (Marshalling Yard) kilichopo Kwala,” alisema Mhe. Kunenge.
Aliongeza kuwa uzinduzi huo ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuwekeza kwenye miundombinu ya kisasa ya viwanda, reli na bandari ili kuongeza tija na ufanisi katika sekta ya uchumi.
Kuhusu Bandari Kavu ya Kwala, Mhe. Kunenge alisema kuwa mradi huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia wastani wa makasha ya mizigo 823 kwa siku, sawa na makasha 300,000 kwa mwaka. Hii itasaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa asilimia 30.
Akifafanua zaidi, alisema kuwa Mhe. Rais Samia atapokea jumla ya mabehewa 160 ya mizigo, ambapo mabehewa 100 ni mapya yaliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya MGR, mabehewa 20 yamefanyiwa ukarabati, na mengine 40 yametolewa na Shirika la Chakula Duniani (WFP).
Kwa upande wa Kongani ya Viwanda ya Kwala, ambayo ni miongoni mwa maeneo ya viwanda makubwa zaidi Afrika Mashariki, Mhe. Kunenge alisema kuwa Mhe. Rais atazindua viwanda saba vilivyokamilika na vinavyoendelea na uzalishaji, pamoja na viwanda vitano ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Kongani hiyo inatarajiwa kuwa na zaidi ya viwanda 250.
Hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, huku Mhe. Rais akitarajiwa pia kufanya mkutano mkubwa na wananchi mara baada ya shughuli za uzinduzi kukamilika.
Miradi inayotarajiwa kuzinduliwa inaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha sekta ya uchukuzi na usafirishaji, na kuifanya Kwala kuwa kitovu cha biashara na uchukuzi wa kimataifa (International Logistic Hub).
Aidha uzinduzi huo utaleta manufa makubwa yakiwemo kuongeza mapato, kukuza usafiri wa Reli, kupunguza uharibifu wa barabara, kutunza manzingira na kuongeza ushindani wa kikanda na Ushirikiano wa kikanda na nchi za jirani kama vile DRC, Zambia, Rwanda,Burundi, Malawi, Zimbabwe, Uganda, na Sudani ya Kusini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.