Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa siku tano kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha huduma zote muhimu zinafikiwa Bandari Kavu ya Kwala ili kurahisisha usafirishaji na huduma kwa watumiaji. Maagizo hayo yalitolewa Julai 31, 2025, wakati wa uzinduzi wa bandari hiyo mkoani Pwani.
Aidha, Rais Samia ameagiza Wizara ya Uchukuzi kushirikiana na sekta binafsi kuhamasisha matumizi ya Bandari Kavu ya Kwala kwa lengo la kupunguza msongamano wa malori Jijini Dar es Salaam. Alisema huduma zitakapokamilika, madereva watapata urahisi kuingia moja kwa moja Kwala bila kusumbuliwa na usafiri mrefu.
Rais alisisitiza kuwa huduma zote muhimu zitakamilike ifikapo Agosti 4, 2025, ikiwemo kuwepo kwa kituo cha polisi na kupunguzwa kwa viwango vya ukodishaji ili kuwavutia wakodishaji wengi. Uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala unatarajiwa kuchochea uchumi wa taifa na kuwavutia wateja wakubwa wa ndani na nje, ikiwa ni pamoja na kampuni kama GSM.
Kuhusu Kongani ya Viwanda ya Kwala, Rais Samia alisema kitatoa fursa kubwa kwa wawekezaji wa ndani na nje kuanzisha viwanda na biashara katika eneo hilo, na akaagiza TRC kuhakikisha mchakato wa uwekezaji haukwamishwi ili kuwezesha matumizi makubwa ya Bandari Kavu ya Kwala. Pia alibainisha mipango ya kuunganisha Bandari Kavu ya Kwala na Bandari ya Bagamoyo na Tanga kupitia reli ya kisasa ya Mwendokasi (SGR).
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema sekta ya uchukuzi ni muhimu katika maisha ya Watanzania na akamshukuru Rais Samia kwa kipaumbele cha uendelezaji wa reli za kisasa. Ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala unazingatia mahitaji ya kiuchumi na kijamii kutokana na upungufu wa uwezo wa bandari kavu 11 zilizopo nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amemshukuru Rais Samia kwa mchango wake mkubwa katika kuleta maendeleo mkoani Pwani. Kunenge alisema tangu 2021 viwanda vimeongezeka kutoka 1,387 hadi 1,681, huku viwanda vikubwa vikiwa 97 kutoka 59, na viwanda vya kati 71 zaidi, na kwamba viwanda hivyo vimeongeza ajira zaidi ya 81,000 kwa pamoja.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alisema mkoani Pwani kuna viwanda vinazalisha bidhaa mbalimbali kama TV, nondo, vioo, magari, saruji, chuma, pamoja na dawa za mifugo na binadamu, jambo linaloonyesha ukuaji wa viwanda na uchumi wa mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.