Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Juni, 2017 amefuturisha wananchi wa Mkoa wa Pwani na kuwataka waumini wa dini ya Kiislam na madhehebu mengine kuendeleza umoja na mshikano uliopo kwa muda mrefu kwa lengo la kudumisha amani nchini.
Mhe. Rais Magufuli amesema anaungana na waumini wa dini ya Kiislamu nchini katika kumi la mwisho la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuwaombea kumaliza kwa amani ibada ya Funga ya Ramadhani ikiwa ni kutekeleza nguzo ya nne kati ya nguzo tano ya dini ya Kiislam.
Amesema kwa mujibu wa dini ya Kiislamu ibada ya Funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni muhimu kwani ni njia sahihi ya kujirekebisha kuachana na matendo maovu yanayoweza kusababisha kutenda dhambi.
‘’Ramadhani ni ibada muhimu kwa Waislaam kwani ndio mwezi ambao huchoma dhambi zao na kutenda matendo mema hivyo ni muhimu kwa ndugu Waislaam kuendeleza yote mema ambayo wanafanya katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kuliombea Taifa.’’
Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Aboubakar Zubeir Ali ametaka wananchi wa Tanzania bila kujali itikadi za kidini kuendelea kuliombea Taifa ili lizidi kuendelea kuwa na amani.
Nae Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Pwani Sheikh Hamisi Mtupa amemshukuru Rais Magufuli kwa ukarimu wake wa kuwaaandalia futari wananchi wa Mkoa wa Pwani ikiwa ni pamoja na makundi maalum ya watoto yatima wa kituo cha Bulome Foundation cha mjini Kibaha mkoani Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.