Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa ametoa kiasi cha dola elfu kumi kwa Mkuu wa chuo cha Kilimo na Mifugo cha Kaole kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani ili kufanya ukarabati wa chuo hicho.
Ametoa kiasi hicho ikiwa kama shukrani yake ambazo amesema zitasaidia kutatua baadhi ya changamoto chuoni hapo.
Rais Mnangagwa alisema hayo mapema Juni 29 alipotembelea iliyokuwa shule ya wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika ambacho hivi sasa ni Chuo cha Kilimo na Mifugo cha Kaole kilichopo Bagamoyo .
Aidha alieleza endapo kutakuwa na uwezekano ataongeza fedha nyingine ili kuongezea kiasi alichotoa kwa ajili ya ukarabati chuoni humo .
Akiwa chuoni hapo alisema yeye ni mojawapo ya waanzilishi wa chuo hicho katika miaka ya sitini akiwa pamoja na viongozi wengine wa nchi za kusini mwa Afrika wakiwemo wa chama cha FRELIMO .
Pia alisema kwamba, alikuwa kiongozi wa ulinzi wa chuo hicho kipindi wakiwa hapa Nchini katika jukumu la kupigania uhuru wa Nchi zao.Aidha alisema wakati huo walikuwa wakisukumwa zaidi na uzalendo kwa Nchi na sio madaraka.
Rais Mnangagwa alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kumpa fursa ya kuitembelea Shule hiyo kwa kuwa ilikuwa ni shauku yake baada ya kuondoka shuleni hapo miaka 58 iliyopita .
"Nimefarijika kutembelea Bagamoyo na kuja Tanzania naamini mwaliko huu utaendeleza mahusiano ya kindugu ya nchi hizi ambao ni wa kipindi kirefu" alisema Rais Mnangagwa.
Aidha aliwashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kumtunza katika kipindi chote alichoishi Bagamoyo hata sasa anajisikia kuwa ni mmojawapo wa jamii ya watu wa wilaya hiyo.
Rais Mnangagwa aliingia Tanzania Juni 28 ambapo alisema Tanzania na Zimbabwe zitaendelea kuimarisha ushirikiano wao .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.