Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta, amefungua rasmi mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa PEPMIS (Watumishi Portal), kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi wa umma katika matumizi sahihi ya mfumo huo, pamoja na upangaji wa majukumu kulingana na taaluma na nafasi zao ili kuongeza ufanisi katika upimaji wa kazi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mchatta alisema mfumo wa PEPMIS ni nyenzo muhimu ya kiutumishi inayosaidia kupanga, kutathmini, na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya kila mtumishi kwa mujibu wa malengo ya taasisi na bajeti husika.
“Ni muhimu kila mtumishi kujiwekea majukumu yanayotekelezeka na kuweka viashiria vinavyoonyesha namna kazi inavyopimwa kwa matokeo,” alisema Mchatta, akisisitiza umuhimu wa kulinganisha majukumu na rasilimali zilizopo katika bajeti ya mwaka wa fedha unaotarajiwa kuanza Julai 2025.
Mafunzo hayo yameratibiwa na wakufunzi kutoka Ofisi ya Rais – Menejiment ya Utumishi wa Utawala Bora ambayo yamehusisha washiriki kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, wakiwemo Wakuu wa Sehemu na Vitengo, Makatibu Tawala wa Wilaya, pamoja na watumishi kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Shirika la Elimu Kibaha, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tumbi, na Shirika la Nyumbu (TATC).
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa yamewasaidia kupata uelewa wa kina kuhusu mfumo huo na umuhimu wake katika kuboresha uwajibikaji na utendaji kazi wa kila mtumishi.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Bi. Moza Mtete, amesema mafunzo hayo yamemwezesha kuelewa namna bora ya kupanga majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji na upimaji wa kazi anazozitekeleza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.