Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Mhandisi Mwanasha Tumbo amewaagiza waratibu na wasimamizi wa fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa unaosimamiwa na Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kuimarisha usimamizi, kuwa waadilifu na waaminifu kwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya wanufaika.
Mhandisi Mwanasha ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha kujadili shughuli za mpango kazi wa Mpango huo kwa mwaka 2021/2022 kilichowahusisha wakuu wa idara na vitengo kutoka Sekretariet ya Mkoa na waratibu wa TASAF wa Halmashauri zote za mkoa wa Pwani.
Alisema kuwa jumla ya kaya za Walengwa 29,683 zinanufaika kupitia mpango huo Mkoani Pwani ambapo sh. Bilioni 5.609 zimeshapokelewa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hivyo ni lazima zisimamiwe ili kutimiza azma ya Serikali na kujiepusha na migongano.
Mhandisi Mwanasha ameeleza kuwa yapo malalamiko kutoka kwa wanufaika Kuwa wakati mwingine fedha hizo haziwafikii, jambo ambalo linachafua mpango mzima wa utekelezaji na akafafanua kuwa malalamiko hayo yanajitokeza kutokana na kuwaachia watendaji na wenyeviti wa vijiji fedha ambapo zinachelewa kuwafikia walengwa.
"Hata huu utaratibu wa Sasa wa kuwalipa walengwa fedha kwenye simu nao una changamoto kwa kuwa walengwa wengine hawajui matumizi ya mitandao ya simu, utakuta mtu anamuagiza mjukuu wake, jirani ama jamaa hadi fedha ikitoka unakuta mlengwa anapata pungufu ama wananufaika ambao hawastahili,” alisema Mhandisi Mwanasha.
Mhandisi Mwanasha aliendelea kusema, "Tuhakikishe kuwa fedha hizi zinawafikia walengwa ili kutimiza azma ya Serikali kusaidia Kaya za Walengwa, Mimi ni shuhuda, nilifika pale Kimaramisale ambako ni kati ya Vijiji vipya vilivyoongezwa kwenye Mpango, tumefika pale watu wakapokea fedha zao na kuishukuru Serikali kwani haijawahi kutokea kwao.”
Kutokana na changamoto hiyo Mwanasha ameelekeza waangalie namna ya kutoa elimu ya Utaratibu huo ili Hali wahusika wapate Uelewa.
Katibu Tawala huyo alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapigania wananchi wa Hali ya chini ili wapate msaada .
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji mkoa , mratibu wa TASAF Mkoani Pwani Roselyn Kimaro alieleza kuwa mbali na kaya kunufaika na fedha, pia ipo miradi 168 yenye thamani ya sh. Bilioni 1.084 iliyoibuliwa na wananchi ambayo inatekelezwa na walengwa na inaendelea vizuri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.