Katibu tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchata amepongeza jitihada za wananchi kuchangia na kushiriki katika usimamizi wa ujenzi wa miradi katika maeneo yao.
Mchata alitoa pongezi hizo wakati alipotembelea wilaya ya Mkuranga leo Mei 4, 2023 na kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea kujengwa kutokana na fedha kutoka halmashauri ya wilaya, wadau wa maendeleo na nguvu za wananchi.
Miradi aliyoitembelea ni paoja na ujenzi wa kituo cha afya Nyamato inayojengwa kwenye kijiji cha Mvuleni pamoja na shule ya Sekondari Kilimahewa inayojenga kwenye kijiji cha Kilimahewa Kaskazini Kata ya Kimanzichana.
Mchata alivutiwa na akapongeza ari ya wananchi kujitolea ambapo katika kituo cha Afya Nyamato wananchi wamechangia nguvu zao kushiriki kutekeleza ujenzi huo, kununua eneo lenye ukubwa wa ekari nne na baadhi yao ni wanakamati ambao wameonesha usimamia vizuri taratibu za ujenzi.
Katika taarifa ya ujenzi wa kituo cha afya Mkanoge iliyosomwa na msimamizi wa mradi huo Abasi Ally Mbwana, mradi huo utagharimu zaidi ya shilingi milioni 400 na tayari majengo matatu ya OPD, maabara na la upasuaji yako kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji.
Mbwana alieleza kuwa kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 15,111 wa vijiji saba vinavyounda kata hiyo ambavyo ni Mkiu, Nyanduturu, Kilimahewa kusini, Kiramba, Tipo, Mkanoge na Mvuleni.
Kwa upande wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Kilimahewa ambayo tayari madarasa saba yenye madawati yamekamilika, wananchi wamechangia zaidi ya shilingi milioni 11, wametoa eneo la ujenzi bila kudai fidia yoyote, wamepanda miti kuhifadhi mazingira na kushiriki katika ujenzi.
Pamoja na pongezi hizo, Mchata alisisitiza wananchi hao kuzingatia kuweka sawa nyaraka za manunuzi na za malipo mbalimbali, kupima maeneo yenye miradi ya serikali na kuwa na hati, kupanda miti ya matunda na ya vivuli.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.