Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Zuwena Jiri amewaasa maafisa wanaohudhuria Mafunzo ya utekelezaji wa Mwongozo wa ushirikiano kati ya wazazi na walimu kutumia maarifa watakayopata kuimarisha ushirikiano kati ya wazazi, walimu, jamii na shule katika mkoa huo.
Akiwa amewakilishwa na Afisa Elimu Mkoa wa Pwani Sara Mlaki na kusoma hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya siku tatu yaliyoanza leo Mach 6, 2023 kwenye ukumbi wa halmashauri ya Mji Kibaha, Zuwena alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Maafisa Elimu wa Wilaya na Kata, Walimu Wakuu na Mwenyekiti wa Kamati ya shule ili waweze kuanzisha, kutekeleza na kusimamia shughuli za ushirikiano wa wazazi na walimu (UWaWa) shuleni.
Aliendelea kusema kuwa mafunzo hayo pia yanalenga kuwawezesha juu ya uongozi wa shule ili waweze kushirikiana katika uongozi na usimamizi kwa ufanisi zaidi ili kuboresha utoaji wa elimu na kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi na kuwa Ushiriki wa Jamii katika Elimu utainua ubora wa elimu kwa kuongeza ushiriki, umiliki, usaidizi wa kuimarisha shule, kuongeza rasilimali na kujengea uwezo wa wazazi na kuimarisha umoja kati ya jamii na shule.
"Umoja huu utasaidia kuboresha ujifunzaji wa darasani na kuwezesha mahusiano kati ya mzazi na mwalimu na hata kusaidia ulinzi na usalama wa mtoto akiwa shule na akiwa nyumbani, Wazazi watapata fursa ya kushiriki katika Elimu ya watoto wao, UWaWa kiwe ni chombo cha kusaida utekelezaji wa majukumu ya Kamati ya Shule ili kuongeza utendaji na usimamizi wa shughuli katika mazingira ya kufundisha na kujifunza," alisema.
Katika mafunzo hayo, washiriki pia wataandaa mipango kazi ili kuwawezesha wana - UWaWa kusaidia katika kuboresha Elimu Mkoani humo.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza (UKAID) kupitia Mradi wa Shule Bora yataendelea kwa viongozi wa elimu katika ngazi ya halmashauri, Kata na Shule zote mkoani Pwani kuanzia Mach 13 - 18, 2023.
Washiriki katika mafunzo hayo ngazi ya Mkoa ni Maafisa wa Elimu Awali na Msingi wa Halmashauri, Waratibu wa Shule Bora ngazi ya Halmashauri, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri, Maafisa Elimu Maalum wa Halmashauri, Wathibiti Ubora wa Shule na Maafisa wa Habari wa Halmashauri.
Wengine ni kundi la wasimamizi na wawezeshaji wakiwa ni Afisa Elimu Mkoa Mkoa, Afisa kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Afisa Elimu Taaluma Mkoa, Muwezeshaji kutoka Chuo Cha Uwalimu Nachingwea, Mratibu wa Shule Bora Mkoa wa Pwani na Timu kutoka Cambridge Education.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.