Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuleta mradi wa umeme vijijini wenye thamani ya zaidi ya bilioni 14.98 mkoani Pwani. Mradi huo unatarajiwa kuboresha maisha ya wananchi na kurahisisha upatikanaji wa umeme vijijini.
Mhe. Kunenge alitoa shukrani hizo leo wakati wa tukio la makabidhiano ya mradi kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na mkandarasi wa mradi, China Railway Construction Electrification Bureau Group (CRCEBG), lililofanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Mradi huo unalenga kunufaisha vitongoji 2,045, ambapo tayari vitongoji 1,135 vimenufaika. Kwa sasa, mradi unaendelea na utawanufaisha wakazi wa vitongoji 135 vilivyobaki, ambavyo vinatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili, kufuatia maelekezo ya Ilani ya CCM inayolenga kufikia upatikanaji wa umeme kwa asilimia 100 kwa wananchi.
Mhe. Kunenge pia ameagiza mradi huo kutambulishwa katika wilaya zote za Mkoa wa Pwani ambazo vitongoji vyake vitanufaika, ili kuwezesha ufuatiliaji na kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa ufanisi.
Aidha, amemshauri mkandarasi wa mradi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kutoa taarifa za changamoto zinazoweza kujitokeza ili zitafutiwe suluhisho haraka.
"Naomba mradi ukamilike kwa wakati, msisukumwe, lakini mkihitaji kusukumwa nitawasukuma, kwani nitawatembelea mara kwa mara," alisema Mhe. Kunenge.
Pia, Mhe. Kunenge amesisitiza umuhimu wa kuharakisha usambazaji wa umeme kwenye maeneo ya visiwani ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa bluu, kuongeza mapato ya serikali, na kukuza sekta ya utalii.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa REA Vijijini, Mhandisi Jones Olotu, alisema kuwa mradi huo unalenga kunufaisha vijiji vyote vya Mkoa wa Pwani ifikapo mwaka 2025.
Afisa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Bi. Felister Edwin, kutoka China Railway Construction Electrification Bureau Group (CRCEBG), akizungumza kwa niaba ya mkandarasi, aliahidi kufanyia kazi maelekezo ya Mkuu wa Mkoa na kuhakikisha mradi unakamilika kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.