Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amepongeza maendeleo ya mradi wa Kivuko cha Nyamisati-Mafia, unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 9. Kivuko hicho kinatengenezwa na kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG) katika eneo la Kimbiji, wilayani Kigamboni.
Kunenge alitoa pongezi hizo Sept 28 ,2024 wakati wa ziara yake ya kukagua hatua za utengenezaji wa kivuko hicho.
Alisisitiza umuhimu wa kivuko hicho kukidhi mahitaji ya wananchi kwa kuzingatia ubora na viwango vinavyohitajika.
"Tumekuja kujua matengenezo yamefikia hatua gani na kuhakikisha ubora na viwango vinakidhi mahitaji ya wananchi," alisema Mhe. Kunenge.
Pia, alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kivuko hicho kwa wakazi wa Mafia na kutoa zaidi ya bilioni 9 kwa ajili ya utengenezaji wake.
"Awali, mradi ulitengewa bilioni 5, lakini kutokana na umuhimu wa kivuko hicho, Rais aliongeza fedha hadi kufikia zaidi ya bilioni 9 ili kuhakikisha kivuko kinajengwa kwa ubora unaohitajika," aliongeza Kunenge.
Baada ya ukaguzi, Kunenge aliagiza mkandarasi kuandaa ratiba mpya itakayowezesha kufanya ukaguzi wa maendeleo ya utengenezaji kulingana na ratiba hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko kutoka TEMESA, Injinia Lukombe Kingombe, alisema kivuko hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 300, magari 10, na mizigo yenye uzito wa zaidi ya tani 120.
Nae Mbunge wa Mafia, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu, Mhe. Omary Kipanga, alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya kivuko hicho, ambacho tayari kimekamilika kwa asilimia 35 ya utengenezaji.
Kivuko cha Nyamisati-Mafia kitakapokamilika kitasaidia kutatua changamoto za usafirishaji kwa wananchi wa Mafia. Kivuko hicho kitakuwa na uwezo wa safari ya masaa matatu kutoka Nyamisati hadi Mafia, pamoja na kuwa na huduma kama sehemu ya kusafirishia maiti, huduma ya kwanza, vyoo, sehemu ya kuhifadhia mizigo ya abiria, na eneo la kulia chakula.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.