Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge ameelekeza Wakala wa ufundi na umeme (TEMESA) kuwasilisha kwa wananchi, serikali ya wilaya na ya mkoa taarifa yenye mpango wao wenye gharama halisi za matengenezo na uwezo wa kivuko kipya kitakachotoa huduma kwa wananchi wa mafia.
Alitoa maelekezo hayo katika kikao cha Bodi ya barabara Mkoa kilichofanyika leo Mach 3, 2023 kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la ofisi yake baada ya kupata maelezo ya Meneja wakala wa ufundi na umeme (TEMESA) Mkoa wa Pwani Mhandisi Rehana Juma alieleza kuwa vivuko vya MV Kilindoni inafanyiwa marekebisho ya kimatengenezo kwa gharama ya zaidi ya sh. milioni 294 na imefikia asilimia 85 ya matengenezo tayari kwa majaribio ili iingie majini kuanza safari zake na kuwa kutokana na matengenezo ya mara kwa mara ya vivuko vilivyopo, Wizara husika na TAMESA imeamua kuanza mchakato wa kununua kivuko kipya chenye uwezo wa kubeba Tani 120 za mizigo na watu 500, kwa thamani ya Sh. Bilioni 9 ili kupunguza adha ya ongezeko la wasafiri wa pande zote mbili za Nyamisati na Mafia.
"Niwaombe TEMESA msifanye usiri katika hili, wananchi wanapaswa kushirikishwa ili nao watoe maoni yao kujua endapo kivuko hicho kitawafaa, haiwezekani leo mnakuja na mpango wenu, na kusema mnaleta kivuko cha zaidi ya shilingi Bilioni 9 wakati hamjashirikisha mkoa, wilaya wala wananchi, muda mwingi wananchi wanakosa usafiri kwa kuwa vivuko vinakuwa kwenye matengenezo na kusababisha abiria kukwama na wanaoathirika zaidi ni wananchi wa wilaya ya Mafia ambao wanauhitaji wa kivuko cha uhakika kitakachoweza kujibu kero ya usafiri na usafirishaji inayowakabali." alisisitiza Kunenge.
Aliendelea kusema kuwa wakati serikali ikiendelea kuufungua mkoa kwa miundombinu mbalimbali ya barabara na reli, pia kuna haja ya kupata ufumbuzi wa muda mrefu kutatua changamoto ya usafiri hasa wa njia ya maji.
Kunenge pia aliitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) nayo kuwasilisha kwa serikali ya mkoa mpango wake wa maboresho yanayohitajika na namna yatakavyotekelezwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mafia Juma Salum alieleza kilio cha usafiri wa uhakika ni mtihani mkubwa kwa wana Mafia akifafanua kuwa sasa ni siku ya tatu wasafiri wa Mafia wamekwama Nyamisati kutokana na kukwama kwa usafiri na kuwa sasa imepita takriban miezi mitano ikiwa kivuko cha MV Kilindoni kikidaiwa kuwa katika matengenezo suala ambalo linakatisha tamaa katika maendeleo ya Mafia.
"Kivuko hiki hakijibu tatizo la usafiri Mafia, tunatakiwa kupata uhakika wa usafiri wa kuingia Nyamisati na Kutoka Mafia, kuwe na mpango wa muda mrefu, kwa shida hizo kunasababisha wananchi kuhitaji huduma ya kivuko cha binafsi kilichokuwepo zamani ili kiwasaidie," alisema Salum.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.