Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, ameielekeza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuhakikisha programu ya IPOSA (Integrated Programme for Out-of-School Adolescents) inakuwa na matokeo chanya kwa kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kuajirika.
Akifunga mafunzo ya walimu wa programu hiyo yaliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano Manispaa ya Kibaha, mkoani humo, alisisitiza elimu inayotolewa kupitia IPOSA haipaswi kubaki kwenye vyeti pekee, bali iwe chachu ya mabadiliko katika maisha ya wahitimu.
“Mradi huu lazima uwe na matokeo ya kweli, vijana wanapaswa kufundishwa stadi zitakazowawezesha kujitegemea kiuchumi, pamoja na kupunguza idadi ya watu wazima wasijua kusoma na kuandika, Hii ndiyo maana halisi ya elimu yenye tija,” alisisitiza Kunenge.
Vilevile Kunenge alimuagiza Afisa Elimu wa Mkoa kusimamia kikamilifu utekelezaji huo na kuhakikisha unaacha alama katika maisha ya vijana wanaonufaika nao.
“Nakuagiza Afisa Elimu Mkoa kuhakikisha kuwa programu ya IPOSA inaleta matokeo yanayoonekana kwa vijana na jamii kwa ujumla, tunahitaji kuona ushahidi wa mafanikio,” alifafanua Kunenge.
Programu ya IPOSA inalenga kuwafikia vijana waliopo nje ya mfumo rasmi wa elimu kwa kuwapatia ujuzi na maarifa mbalimbali, yakiwemo mafunzo ya stadi za maisha, ujasiriamali, kusoma, kuandika, kuhesabu na mafunzo ya amali, ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Mafunzo hayo yamekuwa yakitekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuhakikisha kundi la vijana lisilofikiwa na mfumo wa kawaida wa elimu linapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.