Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ni kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma za afya kwa wazee, ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitambulisho maalum vitakavyowasaidia kutambulika wanapokwenda kupata matibabu na huduma nyingine za msingi wanazostahili.
Kunenge alitoa kauli hiyo Oktoba 2,2024, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, na kuhudhuriwa na wazee mbalimbali pamoja na viongozi wa serikali, dini, na vyama vya siasa.
Alieleza kuwa anatambua mchango mkubwa wa wazee wa Mkoa wa Pwani na ana imani wanaweza kumsemea mazuri Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyofanya katika kuboresha sekta mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuinua maisha ya wananchi wa mkoa huo.
"Mimi kama Mkuu wa Mkoa wa Pwani nimefarijika sana kuwa nanyi katika siku hii muhimu ya maadhimisho ya wazee. Ninawaomba tumpe ushirikiano wa kutosha Rais wetu, kuhakikisha tunamlinda na kumtetea kwa yale yote mazuri anayoyafanya kwa ajili ya nchi hii. Ameweza kutenga fedha nyingi ambazo zimeleta matokeo chanya, hususan katika Mkoa wa Pwani, ikiwemo uongozi wa viwanda nchini," alisema Kunenge.
Aliendelea kufafanua kuwa wazee wa Mkoa wa Pwani wana busara nyingi na wanapaswa kumfariji Rais ili aendelee kuwatumikia wananchi kwa ufanisi. Pia aliahidi kuwaandalia ziara kwa wazee hao kutembelea miradi ya kimkakati ili waweze kujionea na kujifunza kuhusu mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.
Kunenge aliwahimiza wazee kuweka misingi imara ya kumsapoti Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumlinda, kumtunza, na kumtetea katika juhudi zake za kuwatumikia wananchi na kuendeleza miradi ya maendeleo.
Kwa upande wao, baadhi ya wazee, akiwemo Rose Lwanda, Katibu wa Baraza la Wazee katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, waliishukuru serikali lakini walionyesha changamoto ya kutoingizwa kwenye mfumo wa TASAF. Wazee hao waliiomba serikali kuangalia suala hilo ili waweze kupata fursa ya msaada wa TASAF.
Aidha, wazee hao waliiomba serikali kuanzisha mfumo mzuri wa vikundi vya wazee ili waweze kupata mikopo kwa urahisi, jambo litakalowawezesha kujikwamua kiuchumi. Pia walitaka kushirikishwa katika vikao vya maendeleo ili kutoa mawazo yao kwa ajili ya ustawi wa jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.