Mkuu wa Mkoa wa PWANI Abubakar Kunenge ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kuwapatia Wahe. Madiwani wa Halmshauri hiyo Mafunzo ya Uchumi ili waweze kuwa Wabunifu wa vyanzo vipya vya mapato na kutumia Ipasavyo Fursa za Uchumi na Uwekezaji katika Halmshauri yao.
RC kunenge ametoa maelekezo hayo leo Juni 13, 2022 wakati wa Kikao Maalumu cha Baraza la Madiwani cha Kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kilichofanyika Ukumbi wa Magereza Wilayani Mafia.
Katika maelekezo hayo, Mhe. Kunenge amewaeleza madiwani hao kuwa wanatakiwa kwenda na Spidi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambae spidi yake ya kutafuta Wawekezaji imekuwa kubwa na yenye mafanikio.
“Pangeni mikakati Mipya ya Kuongeza Mapato na kukuza Uchumi, kama Mikakati ni ile ile Bajeti ni ile ile hatuwezi kuwa na matokeo mapya kwa kuwa Bajeti ni mipango unayoipa gharama. Amesema RC Kunenge.
Ameeleza kuwa Zamani Halmashauri zilikuwa zinapata Ruzuku Kubwa lakini kwa sasa Serikali imewapa Miradi Mikubwa ya Kimkakati na halmashauri kutakiwa kuibua vyanzo vipya Ili iweze kujiendesha.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani pia alitumia nafasi hiyo kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kupata Hati safi kwa Miaka 6 Mfululizo lakini akaitahadharisha kuwa Kupata hati safi ni kwa Mujibu wa Mahesabu waliyotayarisha na kwamba halmashauri iwasaidie Wananchi kupata huduma.
Akigusia juu ya Migogoro ya Ardhi kwenye Halmashauri hiyo, Mhe. Kunenge amesema kuwa ameombea fedha Serikali Kuu ili kisiwa hicho kipimwe na kupangwa na akautaka Uongozi wa Halmshauri hiyo kuwaandaa Wananchi na Mabadiliko Makubwa ya kiuchumi kisiwani hapo.
"Tunataka kisiwa hiki kiwe eneo zuri sana baadhi ya vitu tulivyonavyo tunaongoza Duniani, Mafia ni Lulu” amesema Kunenge.
Kuhusu hoja za ukaguzi, RC Kunenge amemwelekeza Katibu Tawala Mkoa kufuatilia zile zote zilizojirudia na kuwachukulia hatua wote waliosababisha Hoja hizo na akaitaka Halmashauri hiyo kufunga Hoja zote zilizo ndani ya Uwezo wao ifakapo Septemba 30 na kupitia Sheria ndogo na kufanya marekebisho.
Aidha kuhusu Changamoto ya madaktar na wahudumu wa Afya amemwelekeza Mganga Mkuu wa Wilaya kuanza mpango wa Hospital inayotembea (Mobile Clinic) wakati Serikali ikiwa inatafutia Ufumbuzi Changamoto hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmshauri hiyo Juma Salum Ally amempongeza Mkuu huyo wa Mkoa kwa kuitangaza Mafia, amesema kuwa wamefanikiwa kudhibiti Ukusanyaji wa Mapato ambapo wameongeza kutoka Shilingi Milioni 900 walizokuwa wanakusanya mwaka jana hado Bilioni 1.3 mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.