Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ameiagiza idara ya elimu mkoa kusimamia kikamilifu Shule Maalum ya Sekondari ya wasichana wenye vipaji ya Bibi Titi Mohammed iliyopo Utete Rufiji ili iwe mfano wa kuigwa kwa kutoa elimu na ufaulul wa juu kati ya shule kumi maalum za Sekondari za wasichana zilizojengwa na Serikali nchini.
Akipokea vitanda 40 vilivyogharimu shilingi milioni 12 kutoka Benki ya NMB kwa malazi ya wanafunzi 80, sanjali na makasha ya maziwa kutoka kampuni ya ASAS, Kunenge alieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anaonyesha jitihada kuboresha sekta ya elimu, hivyo idara ya elimu haina budi kusimamia jitihada hizo.
"Rais amedhamiria kuboresha mazingira ya sekta ya elimu na tayari ameanzisha shule za Sekondari maalum za wasichana kumi ambapo nyingine 16 awamu ya pili zitajengwa nchi nzima kufikia idadi ya shule 26, pia shule za Msingi 219 na za Sekondari 718 zimejengwa," alifafanua Kunenge.
RC Kunenge pia ameielekeza Halmashauri ya wilaya ya Rufiji kupanga Mji katika eneo palipojengwa shule hiyo ya Bibi Titi Mohamed ili Mji ukue.
Akikabidhi vitanda hivyo, Mkuu wa Matawi na Mauzo wa Benki ya NMB Donatus Richard, ameeleza kuwa wametoa vitanda 40 ikiwa ni sehemu ya asilimia moja wanayorejesha kwa jamii kutoka kwenye faida.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle ametoa shukrani kwa Serikali kwa ujenzi wa shule ya Sekondari Bibi Titi Mohammed ambayo imegharimu shilingi Bilioni 4.1.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.