Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewataka waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha miradi yote iliyochini ya mfuko huo inakamilika kwa wakati na kuendana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Kunenge ametoa kauli hiyo leo Septemba 15, 2023 wakati akifungua kikao cha mwaka cha kujadili utekelezaji wa shughuli za TASAF (III) awamu ya pili ambapo alipokea taarifa pamoja na kutoa tuzo kwa Halmashauri ambazo zimefanya vizuri kwenye miradi mbalimbali.
Amesema, Serikali imetoa fedha nyingi kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wananchi ikiwemo Ujenzi wa Shule, maji, barabara na kilimo lakini kumekuwa na changamoto ya miradi hiyo kutokamilika kwa wakati.
Amesema kitendo cha baadhi ya miradi kutokamilika kwa wakati kinamkera Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu linakwamisha lengo la kuwahudumia wananchi wake hususani wanaotoka katika kaya masikini.
“Mfuko huu unasimamiwa moja kwa moja na Ofisi ya Rais na amefanya hivyo kwa sababu ya umuhimu na uzito wa jambo hili, sasa inaumiza kuona fedha nyingi anazozitoa kwa ajili ya kukamilisha miradi inasuasua, sambamba na walengwa wa mfuko huo kutonufaika kwa sababu ambazo hazina tija, waratibu wote wa TASAF katika kila wilaya za mkoa huu, simamieni kikamilifu suala hilo hili,” amesema Kunenge.
Aidha amewataka maofisa wanoshughulika na mifumo ya utunzaji kumbukumbu za wanufaika wa TASAF kuwaondoa wanufaika ambao tayari wameondoka kwenye umasikini uliokithiri baada ya kuwezeshwa ili wengine waingizwe kwenye Mpango huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.