Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kuepuka kuzalisha hoja za ukaguzi kwa kuandaa mipango na bajeti kwa kuzingatia vipaumbele vinavyolenga kuwandolea wananchi kero na kuwapatia maendeleo.
Maagizo hayo ameyatoa leo Juni 19, 2023 kwenye kikao maalum cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kilichoketi kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali - CAG kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo wilaya hiyo imepata hati safi.
Amesema kuwa hakuna sababu ya halmashauri kuzalisha hoja iwapo utekelezaji wa shughuli mbalimbali utazingatia na kufuata taratibu zote kwa mujibu wa mipango na bajeti na akaielekeza halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa hoja zote 38 kati 62 zilizopitiwa na kutolewa dosari na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali CAG mwaka wa fedha 2021/2022 zinapatiwa majibu kwa haraka ili ziweze kufungwa.
“Hakikisheni hoja hizi 38 ambazo bado hamjazijibu ikiwa ni pamoja na ya ukusanyaji mapato na uhaba wa wakaguzi wa ndani mnazitolea maelezo haraka ili kupata ufumbuzi wa masuala ambayo yanakwamisha utekelezaji wa shughuli za kuwaletea wanchi maendeleo,“ amesema Kunenge.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashid Mchata amewashauri viongozi wa Wilaya hiyo kujipanga, kuhakiki na kuandaa nyaraka na kuzitafutia majibu hoja zote kabla ya mwezi Desemba ili kurahisisha zoezi la ukaguzi wa CAG.
Awali akiwasilisha ripoti ya CAG, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Michael Gwimile amemuahidi, Mkuu huyo wa Mkoa kushughulikia dosari zote zilizobainika kwenye ripoti hiyo.
Naye Mkaguzi Mkuu wa nje kutoka ofisi ya CAG Mkoa wa Pwani Mary Dibogo ameishauri Halmashauri hiyo kuongeza idadi ya wakaguzi wa ndani kwa ajili ya kushughulikia na kudhibiti mapema dosari ambazo zinaweza kubainishwa na CAG.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.