MKuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge ameiagiza Halmashauri ya Rufiji kutoa majibu kuhusiana na hoja za ukaguzi wa hesabu ambazo hazijafungwa hadi sasa kabla ya June 30.
Kunenge ametoa maagizo hayo Juni 15 kwenye baraza maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya Rufiji la kujadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka 2019/2020.
Taarifa ya maagizo hayo imetolewa na mkuu wa Wilaya ya Rufiji Kanal Patrick Sawala kwa niaba ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani.
"Kuna baadhi ya hoja ambazo ziko ndani ya uwezo wa Halmashauri na hazijafungwa hadi sasa, zote hizo zinatakiwa kutolewa sababu za kuchelewa kabla ya kuanza mwaka mwingine wa ukaguzi haujaanza; hoja hizo zinatakiwa kutolewa maelezo ya kutosha ili Mkaguzi wa hesabu azifunge," amesema Kunenge.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu na zilingane na ukubwa wa hasara kwa mtumishi yeyote aliyesababisha hasara kwa Halmashauri.
"Kwenye taarifa yenu nimeona kuna watumishi wamekusanya fedha bila kuzifikisha benki kiasi cha Shilingi 189,249,365 ninaagiza fedha hizo zirudishwe kabla ya June 30 na watumishi husika wachukuliwe hatua" alisisitiza.
Wakati huo huo Kunenge ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza na kuchukua hatua kwahoja ambazo hazijafungwa hadi sasa na taarifa ifike ngazi ya mkoa kabla ya June 19.
Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Mwanaasha Tumbo amewataka watumishi kufuata kanuni, taratibu na kanuni miongozo kuepuka kuobua hoja mpya.
Tumbo amesema kama Halmashauri inapata hati safi hakuna sababu ya kuwa na hoja ambazo hazijajibiwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rufiji Juma Ligomba amemuomba Katibu Tawala wa Mkoa huo kufanya utaratibu wa kuongezewa mkaguzi wa hesabu kwani kitengo hicho kina mtumishi mmoja.
Ligomba amesema kwa miaka tisa mfululizo Halmashauri hiyo imekuwa ikipata hati safi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.