Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, amewataka TEMESA kushughulikia kwa wakati maoni ya wadau zikiwemo taasisi za watu binafsi ambazo hufika ofisini kwao kwa ajili ya kupata huduma.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Meja Edward Gowelo alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge kwenye kikao kilichowahusisha TEMESA na wadau wake zikiwemo Taasisi za serikali na za watu binafsi kilichofanyika Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani.
Kwenye kikao hicho, Mkurugenzi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA, Lazaro Kilahala amesema katika kuhakikisha wanaboresha huduma zao tayari wanazo karakana 21 nchini ambazo zinatoa huduma kwa ubora unaotakiwa huku 13 zikifanyiwa marekebisho.
Amesema majukumu ya TEMESA ni kufanya matengenezo ya magari, pikipiki, usimikaji wa mitambo ya umeme, kusimamia na uendeshaji wa vivuko na kukodisha mitambo ya ujenzi.
Ameongeza kuwa tayari wamekamilisha vivuko 32 nchini ambavyo vinafanya kazi na wananchi wanapata huduma muda wote lakini pia wanaendelea na maboresho ya upatikanaji wa huduma.
Amesema serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kusaidia wakala huyo kutoa huduma nzuri kwa wananchi hivyo anategemea wataendelea kuboresha kulingana na mahitaji wa watu.
Akibainisha maboresho yanayofanyika kwenye taasisi hiyo, Mkurugenzi wa Matengenezo wa TEMESA Hussein Hassan amesema kuwa wamechukua uamuzi wa kuwapeleka mafundi wake 50 kwenye vyuo mbalimbali kujifunza mbinu za kisasa za utengenezaji wa vyombo vya moto ili kuepusha malalamiko kwa wateja wao.
Hassan amesema wameamua kuwapeleka vyuoni mafundi hao baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wateja wakidai baadhi ya magari yanashindwa kutengenezwa ipasavyo au kuchelewa kutokana na matoleo mbalimbali ambayo upatikanaji wa vifaa vyake ni changamoto na utengenezaji wake unahitaji ujuzi zaidi.
Kutokana na hali hiyo, amesema wamepeleka vyuoni kujifunza na baada ya kuhitimu watakuwa mafundi wazuri ambao wataweza kutengeneza magari kwa ubora unaotakiwa na kwa muda mfupi ukilinganisha na ilivyokuwa awali.
“Hatua hii ni sehemu ya maboresho yetu, sisi TEMESA kupitia kitengo chetu cha huduma kwa wateja tulipokea maoni mengi likiwemo suala la uchelewaji wa ukarabati na utengenezaji wa magari, ifahamike kuwa kila mara kunakuwa na matoleo mapya ya magari, sasa ili tukidhi mahitaji ya wateja wetu ni vyema tukawa na ujuzi na teknolojia ya kutosha ili kila gari tuweze kulihudumia,” amesema Hassan.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.