Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kusimamia upangaji wa Wafanyabiashara kwenye jengo jipya la soko la Utete ambalo ujenzi wake umegharimu Sh. Milioni 172.
Akizungumza na wananchi wa Utete wakati akizindua soko hilo leo April 27, 2023, Mhe. Kunenge alitoa maelekezo hayo ili wananchi wanaohitaji kuendesha shughuli zao za kujipatia kipato katika soko hilo wasikumbane na adha ya kusumbuliwa na madalali wakati wa kuomba kupangiwa maeneno na vizimba mahala hapo.
Mhe. Kunenge ameeleza kuwa ujenzi wa Soko hilo lenye Vizimba 89 na matundu 7 ya vyoo ni mafanikio makubwa katika kuanzisha, kujenga, kuendeleza na kuboreha miradi ya maendeleo ambayo serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inatekelezo na hivyo ni matarajio yake kuwa litawanufaisha Wananchi wa Utete kwa kuwa hiyo ni sehemu ya huduma.
"Mhe. Rais anafanya kazi kubwa ili kuboresha maisha ya Wananchi wa Tanzania mkiwemo na wana-Rufiji, analeta fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ya Masoko, Miundombinu ya Barabara, maji, vituo vya huduma za afya na elimu, itunzeni ili idumu na kutoa huduma endelevu," alisema Kunenge.
Uzinduzi wamradi wa soko hilo umefanyika ikiwa ni muendelezo wa kuzindua miradi ya Maendeleo ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kunenge amemtaka Mkurugenzi wa Halmshauri ya wilaya ya Rufiji kuanza kupanga Mji wa Utete kwa kuwa mji huo ni Mji mzuri na unaokuwa kwa kasi. Pia amewaasa wazazi, walezi na jamii kusimamia suala la maadili kwa kutunza na kulea watoto ili wasijiingize katika tabia na tamaduni zisizoakisi maadili ya kitanzania.
Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa pia alikagua miradi mbalimbali ya maji, afya na elimu katika halmashauri za Rufiji na Kibiti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.